Mbunge wa Viti Maalum Esther Bulaya amesisitiza kuwa yeye bado ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), isipokua suala la yeye kufukuzwa uanachama ni mambo ya ndani ya chama na ndio maana mpaka leo wanapigania haki yao ya kuwa wanachama wa Chadema.
Bulaya ameyasema hayo leo kwenye mahojiano maalum na chombo cha habari cha Clouds Media, ambapo ameeleza kuwa yeye na wenzake 18 waliofukuzwa uanachama waliamua kwenda Mahakamani kudai uhalali wao wa kuwa wanachama baada ya maamuzi ya vikao vya ndani ya chama.
“Mimi ni mpinzani sio CCM tena wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA. Suala la kunifukuza hayo ni mambo ya ndani ya vyama. Na ndio maana sisi tumesema ni Wana- CHADEMA tulikwenda kutetea Uana-CHADEMA wetu” amesisitiza Bulaya.
Itakumbukwa kuwa Novemba 27,2020, Ester Bulaya na wenzake 18 wakiongozwa na Halima Mdee walifukuzwa uanachama wa Chadema kwa kile kilichoelezwa wamekiuka Kanuni na Katiba ya chama hicho kwa uamuzi wao wa kwenda Bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa Viti Maalum bila chama hicho kupitisha majina yao kama wabunge wa viti maalum.
Katika mahojiano hayo Bulaya amesema madai ya kwamba waliingia bungeni bila idhini ya chama na kwamba walifoji kuingia ndani ya bunge kwa bendera ya Chadema si kweli kwa kuwa huwezi kuingia bungeni bila bendera ya chama na utaratibu ulifanyika kupitia ofisi ya Katibu Mkuu ambayo inaelezwa kwamba ilipeleka majina yao
“Kwanza hakuna mtu yoyote anayeweza kuingia bungeni bila bendera ya chama. Kwa unavyonijua Mimi Ester Bulaya Mimi sio chizi, yaani nitoke huko nimekurupuka nikaenda kuapa bungeni. Na hakuna aliyefoji kuingia bungeni. Utaratibu wa kawaida ulitumika ofisi ya Katibu mkuu ilipeleka majina.Ni kama kawaida nilivyoapa kuwa Mbunge wa Viti Maalum nikiwa CCM, niligombea majina yanapelekwa tume unatangazwa. Na ofisi ya Katibu mkuu ndio yenye ridhaa ya kupeleka majina. Iliyosaini ni ofisi ya Katibu mkuu”– Ester Bulaya, Mbunge Viti Maalum.
Mbali na hayo Bulaya ameunga mkono kampeni ya Chadema ya “No Reforms No Election” kutokana na mazingira ya uchaguzi yaliyoshuhudiwa katika changuzi zote zilizofanyika nchini kwamba kwa sasa kinachohitajika ni mabadiliko ya mfumo ya uchaguzi ili kuhakikisha haki inapatikana kupitia uchaguzi huru na haki.
“Tunataka uchaguzi kama ulivyofanyika kwenye chama chetu, aliyeshindwa ampongeze aliyeshinda.Freeman Mbowe alikubali matokeo na kumpongeza Tundu Lissu. Hayo ndiyo tunayoyataka kwenye uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa,” alisisitiza Bulaya.
Kwa sasa hatma ya Bulaya na wenzake ipo chini ya Baraza Kuu ambalo kimsingi ndio litakaloamua uanachama wao baada ya Mahakama kutoa nafasi kwa chama kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.