Bunge la Marekani laidhinisha muswada wa kutathmini upya uhusiano wake na Tanzania

Kamati ya Mahusiano ya Kigeni yabunge la Marekani imeidhinisha miswada mitano ya sera za mambo ya nje, ikiwemo muswada unaotaka kufanyika kwa tathmini ya kina ya uhusiano kati ya Marekani na Tanzania kufuatia kile wabunge wa Marekani wanachokitaja kuwa kuongezeka kwa vurugu za kisiasa na kudorora kwa demokrasia nchini humo.

Mjumbe Mkuu wa Upinzani katika kamati hiyo, Seneta Jeanne Shaheen wa chama cha Democratic, amesema uungwaji mkono wa pande mbili za kisiasa kwa miswada hiyo unaonesha dhamira ya kuimarisha usalama wa taifa la Marekani na kuendeleza ushawishi wake duniani.

Muswada unaohusu Tanzania, uliowasilishwa kwa ushirikiano na Seneta Ted Cruz wa chama cha Republican, unaitaka serikali ya Marekani kufanya tathmini ya kina ya mahusiano ya nchi hizo mbili. 

Aidha, utaitaka Washington kuchunguza kwa karibu uhusiano unaozidi kuimarika kati ya Tanzania na mataifa ya China na Urusi, pamoja na athari zake kwa maslahi ya Marekani katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mbali na Tanzania, kamati hiyo pia imeidhinisha muswada wa kusaidia nchi washirika kupata teknolojia za kidijitali za Marekani kwa lengo la kupunguza utegemezi wa teknolojia za China.

Wabunge hao pia wamepitisha sheria inayolenga kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za walipa kodi wa Marekani zinazotumika kufadhili misaada ya kigeni, hasa bidhaa za chakula na vifaa vya uzazi wa mpango vinavyotolewa kwa nchi mbalimbali.

Katika hatua nyingine, kamati hiyo imeunga mkono kufutwa kwa baadhi ya vikwazo dhidi ya Syria vilivyowekwa wakati wa utawala wa aliyekuwa rais Bashar al-Assad. Wabunge wanaounga mkono hatua hiyo wanasema inaweza kusaidia juhudi za ujenzi upya wa Syria na kupunguza ushawishi wa China na Urusi nchini humo.

Kamati hiyo pia imeidhinisha muswada wa usalama wa eneo la Arctic unaolenga kukabiliana na shughuli za ujasusi na ushawishi wa mataifa ya kigeni, hasa kufuatia kuongezeka kwa ushirikiano kati ya Urusi na China katika eneo hilo.

Miswada hiyo sasa itawasilishwa katika hatua zinazofuata za mchakato wa kutungwa sheria kabla ya kuanza kutumika rasmi.