Bunge la Ulaya laitaka Tume ya Ulaya kusitisha msaada wa euro milioni 156 kwa Tanzania

Wabunge wa Bunge la Ulaya wamepitisha azimio linaloitaka Tume ya Ulaya kuondoa pendekezo lake la kutoa msaada wa euro milioni 156 kwa Tanzania katika mwaka 2026, wakieleza kuwa hali ya haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria nchini bado inatia wasiwasi.

Azimio hilo lilipitishwa leo Alhamisi kwa kura ya kuonyesha uungwaji mkono bungeni, likihusu uamuzi wa Tume ya Ulaya wa kufadhili Mpango wa Hatua wa Mwaka wa 2026 kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika azimio hilo, wabunge wa Ulaya walikumbusha kuwa mwezi Novemba 2025 Tume ya Ulaya ilisimamisha kwa muda mchakato wa kuidhinisha ufadhili huo kufuatia wasiwasi mkubwa uliotolewa na wabunge kuhusu mwenendo wa uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025, ambao waliutaja kuwa na dosari kubwa, pamoja na hatua za serikali kukabiliana kwa nguvu maandamano yaliyofuata baada ya uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa azimio hilo, maandamano hayo yaliripotiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 400 huku mamia ya wengine wakikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Hata hivyo, wabunge hao wamesema kuwa wasiwasi waliowahi kuwasilisha kupitia maazimio mbalimbali kuhusu mwenendo wa serikali ya Tanzania haukuzingatiwa ipasavyo katika uamuzi wa kuendelea na mchakato wa kuidhinisha ufadhili wa mwaka 2026.

Miongoni mwa hoja zilizotolewa ni kile walichodai kuwa ni kuendelea kwa serikali ya Tanzania kuahirisha ziara ya ujumbe wa Wabunge wa Ulaya kutoka Kamati Ndogo ya Haki za Binadamu. Kwa mujibu wa wabunge hao, hatua hiyo imezuia ujumbe huo kutembelea Tanzania kwa lengo la kujadili masuala ya haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria.

Wabunge wa Ulaya pia wameeleza kuwa rasimu ya uamuzi wa Tume ya Ulaya kuhusu ufadhili huo inazidi mamlaka iliyopewa tume hiyo na kwamba haipatani na sheria za Umoja wa Ulaya.

Kutokana na hali hiyo, wameitaka Tume ya Ulaya kuondoa rasimu hiyo ya uamuzi inayohusisha msaada wa euro milioni 156 na kuwasilisha pendekezo jipya litakalozingatia masuala ya haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria.

Hata hivyo, wabunge hao wamesisitiza kuwa mabadiliko yoyote katika mfumo wa ufadhili yasije kuathiri utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi, ulinzi wa haki za binadamu au msaada kwa mashirika ya kiraia.

-Kiini hasa ni kipi?-

Bunge la Ulaya linaeleza kuwa baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025, ambao baadhi ya wadau waliutaja kuwa haukuwa wa haki na huru, serikali ya Tanzania ilikabiliwa na tuhuma za kutumia nguvu dhidi ya maandamano ya wananchi.

Kwa mujibu wa azimio hilo, Tume ya Taifa ya Uchunguzi iliyoundwa kuchunguza matukio ya vurugu yaliyohusiana na uchaguzi ilitangaza Aprili 23, 2026 kuwa watu wasiopungua 518 walipoteza maisha. 

Hata hivyo, tume hiyo haikutaja waliowajibika wala kuchapisha hadharani ripoti yake kamili, jambo ambalo wabunge wa Ulaya wanasema limeathiri juhudi za uwajibikaji na upatikanaji wa haki kwa waathirika.

Aidha, wabunge hao walikumbusha kuwa Mei 8, 2025 walipitisha azimio jingine kuhusu kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu. Katika azimio hilo, walilaani kukamatwa kwake na kueleza wasiwasi kuhusu mashtaka ya kisiasa dhidi yake ambayo yanaweza kupelekea adhabu ya kifo.

Bunge la Ulaya lilitaka serikali ya Tanzania kumuachilia huru mara moja na bila masharti Tundu Lissu, huku likisisitiza haki yake ya kupata usalama, uwakilishi wa kisheria na kusikilizwa kwa kesi yake kwa haki.