Bunge la Zambia Lapitisha Kwa Utata Muswada wa Kubadili Sheria za Uchaguzi

Bunge la Zambia limepitisha muswada tata wa sheria unaolenga kubadilisha vifungu vya katiba vinavyohusiana na uchaguzi, hatua ambayo upinzani unasema itampa nguvu Rais Hakainde Hichilema katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Bunge la Zambia Lapitisha Kwa Utata Muswada wa Kubadili Sheria za Uchaguzi

Wanasiasa wa upinzani, asasi za kiraia pamoja na makundi ya kidini walipinga vikali Muswada wa 7 (Bill 7), wakidai kuwa uliharakishwa kupitishwa bungeni na kwamba utamnufaisha Rais Hichilema na chama chake cha United Party for National Development (UPND) katika uchaguzi wa Agosti 2026.

Muswada huo unapendekeza kurekebisha baadhi ya vifungu vya katiba ya taifa hilo lenye utajiri wa shaba kusini mwa Afrika, ikiwemo kuongeza idadi ya viti vya wabunge wanaochaguliwa pamoja na kutenga viti 40 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Aidha, muswada huo unapendekeza kuondoa kikomo cha mihula miwili ya miaka mitano kwa mameya.

Akizungumza baada ya zoezi la kupiga kura kwa wabunge kukamilika,Waziri wa Sheria, Princess Kasune, alisema muswada huo ni “ahadi kwa wananchi wa Zambia ya kuimarisha haki na usawa.”

Muswada huo sasa unasubiri kutiwa saini na Rais Hichilema ili uwe sheria.

Kwa upande wake, mbunge wa upinzani kutoka chama cha Patriotic Front (PF), Francis Kapyanga, alisema hatashiriki “kuhalalisha jambo lisilo halali.”

Mvutano wa kisiasa nchini humo, yenye wakazi takribani milioni 22, umeendelea kujitokeza, ikiwemo sintofahamu kuhusu mazishi ya aliyekuwa rais mtangulizi wa Hichilema kutoka chama cha PF, Edgar Lungu, aliyefariki dunia mwezi Juni akiwa hospitalini nchini Afrika Kusini.

Familia ya Lungu imekataa kuurejesha mwili wake nchini kwa ajili ya mazishi kwa sababu Rais Hichilema alitaka kuongoza shughuli za mazishi hayo.

Akizungumzia kupitishwa kwa Muswada wa 7, msemaji wa familia ya Lungu na pia mgombea urais anayetajwa wa chama cha PF, Makebi Zulu, aliandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba, “Mapambano ya demokrasia na heshima ya utawala wa sheria yanaanza rasmi leo.”

Rais Hichilema, ambaye anatarajiwa kuwania muhula wake wa pili na wa mwisho wa miaka mitano kwa mujibu wa katiba, alikiri kuwa muswada huo “umejaribu mshikamano wa kitaifa,” lakini akasisitiza kuwa uamuzi wa bunge unapaswa kuheshimiwa.