CAG Kichere kuanza ukaguzi wa fedha za COVID-19

Rais Samia Suluhu Hassan, akipokea Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/2021 kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma jana tarehe 30 Machi, 2022.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ameanza kukagua fedha za Covid-19 ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa fedha hizo.

CAG Kichere aliyasema hayo wakati anakabidhi ripoti yake ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2020/2021 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma jana, Machi 30,2022.

Kichere alisema serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendeleo chini ya Mpango wa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19, hivyo katika kuunga mkono jitihada hizo za serikali, ameanza kukagua fedha zote za mradi huo shilingi trilioni 1.3.

Alisema lengo la ukaguzi huo ni kutekeleza maelekezo ya Rais Samia ya kuhakikisha fedha zote hizo zinatumika kama ilivyopangwa.

“Ninaendelea na ukaguzi katika maeneo yote yaliyopatiwa fedha za mradi wa Covid-19 Tanzania. Nakuahidi Mheshimiwa Rais kwamba kila senti ya fedha hiyo itakaguliwa kwa kuhakikisha zimetumika kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo husika,” alisema Kichere.

Aliongeza: “Mheshimiwa Rais, nitakapokamilisha ukaguzi huu nitawasilisha ripoti kwako na matokeo yake yatawekwa hadharani ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa fedha hizo, hii inazingatia maelekezo yako uliyoyatoa siku unazindua mradi huu.”

Hata hivyo akizungumza mara baada ya kupokea ripoti Rais Samia alisema hatarajii kwamba CAG atasubiri hadi mwakani ndipo amkabidhi ripoti ya uchunguzi huo.

Sambamba na fedha za Covid-19, Kichere alisema ameanzisha pia ukaguzi wa fedha na utaratibu wa kesi zilizohitimishwa kwa kufuata sheria ya makubaliano ya kukiri kosa ya mwaka 2019 ili kujiridhisha na taratibu zote na kiasi kilichokusanywa kutokana na utaratibu huo.

Kwa mujibu wa Kichere, ukaguzi huo pia utahusisha mali zilizotaifishwa na serikali.