Search
Close this search box.
Africa
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kitaitisha kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambacho kitawaita na kukutana na mawaziri wote kupitia Baraza la Mawaziri, kwa ajili ya kujadili na kutafuta majawabu kuhusu hali ya maisha ya Watanzania, kwa kuzingatia mwenendo wa uchumi nchini na duniani.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Tanzania Bara, Ndugu Abdulrahman Kinana, Aprili 10, 2022, alipokuwa akizungumza na viongozi na baadhi ya wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kwenye mkutano wa kumpokea na kumpongeza kwa kuchaguliwa na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika Aprili 1, 2022 jijini Dodoma, kushika dhamana hiyo.

“Ningependa kurudia au kuelezea kauli ya Mwenyekiti wa Chama na Rais, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Chama (maalum) wa CCM Dodoma, alitoa kauli. Rais alisema hivi, kwamba muda si mrefu, katika muda mwafaka ataitisha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Maalum. Na katika kikao hicho atawaita na mawaziri. Lengo ni moja, kwa namna alivyoeleza Mwenyekiti wetu na Rais, kujadili hali ya uchumi wa nchi yetu.

“Kuangalia namna tutakavyoharakisha maendeleo ya wananchi. Kuangalia namna tutakavyoshughulika na mipango ya wananchi. Kuangalia hali ya maisha kwa ujumla ya Watanzania. Kwa sababu Rais amesikia mara kadhaa juu ya suala la ugumu wa maisha. Hivyo lazima tukae, tufanye uchambuzi, tuone. Na kikao hicho Mwenyekiti wake atakuwa si mwingine, ila ni Mwenyekiti (wa CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Ndugu Kinana na kuongeza;

“Si mara nyingi katika historia ya chama chetu, Halmashauri Kuu inakaa pamoja na mawaziri. Lakini rais kwa kuona umuhimu wa jambo hili, ameamua kuwa kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu. Kazi ya Halmashauri Kuu ni kutengeneza sera, kusimamia utekelezaji wa sera, kuandaa ilani na kusimamia ilani. Kazi ya Baraza la Mawaziri ni kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kutekeleza ahadi tulizowapatia wananchi na kusimamia maendeleo ya Watanzania.

“Makundi haya mawili yakikaa pamoja, chini ya uongozi wa Mwenyekiti na Rais Samia Suluhu Hassan nina hakika tutatoka na majawabu mazuri ya kusaidia maendeleo ya Watanzania,” amesema Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Ndugu Kinana.

Aidha, ametumia mkutano huo kutoa kauli ya CCM kumthibitishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa CCM kinashikamana naye kumsaidia kutekeleza wajibu wake kwa wananchi, huku pia akiwataka wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla, kuendelea kumuunga mkono Rais Samia ambaye ana nia njema na maono mazuri katika sekta zote zinazohusika kuweka mazingira ya wananchi kujiletea maendeleo, ikiwa ni pamoja na kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kinana pia ametoa wito kwa wanachama wote wa CCM kujitokeza kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Chama hicho ambao umeanza mwezi huu, hasa akitoa wito kwa makundi ya vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali kwa kuzingatia sifa walizonazo kwa mujibu wa Katiba, Kanuni, Miongozo na taratibu mbalimbali za CCM.

Comments are closed