Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Nchimbi, amekanusha vikali madai kwamba chama chake kinahusika na matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini Tanzania. Nchimbi alisisitiza kuwa vitendo hivi vinachochewa na magenge ya uhalifu yenye lengo la kutafsiri CCM kama wauaji na kuchochea ugumu wa uhusiano kati ya chama hicho na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Nchimbi alieleza kwamba, “Mwanachama wa CHADEMA alitekwa na kuuawa kikatili siku chache zilizopita, jambo ambalo ni la kusikitisha sana. CCM tunalaani vikali vitendo hivi na tunasisitiza kwamba Ilani yetu ya CCM ukurasa wa 156 inasema kwamba tutaliwezesha Jeshi la Polisi kudhibiti usalama wa raia na mali zao.”
Nchimbi aliongeza kwamba, “Mtu yoyote anayeshiriki katika utekaji au mauaji ya raia anafanya hivyo kwa lengo la kuharibu taswira ya CCM mbele ya umma. Ni watu wenye nia mbaya wanajihusisha na vitendo hivi na hawawezi kuwa na nia njema na CCM.”
Nchimbi aligusia pia kauli ya Mbowe, kiongozi wa CHADEMA, ambaye ameweka muda wa mwisho kwa serikali kuwataja wahusika wa matukio haya maovu. “Mbowe, ambaye ni rafiki yangu mwenye hekima, ametoa muda wa mwisho kwa Rais, ikifika Septemba 23, 2024 ikiwa wahusika hawajatolewa, hatua zitachukuliwa. Tunapaswa kushirikiana, CCM na upinzani, kuhakikisha kuwa genge la watekaji halifanikiwi kutufarakanisha,” alisema Nchimbi.
Katibu Mkuu huyo pia amewataka wananchi kuwaamini polisi na kutambua jitihada zinazofanywa na vyombo vya usalama. Aliongeza kwamba, “Katika miaka mitano iliyopita, polisi 42 wameuawa katika mapambano na majambazi, na 141 wamejeruhiwa. Polisi wanafanya kazi kubwa na tunapaswa kuunga mkono juhudi zao.”
Nchimbi alisisitiza umuhimu wa kuondoa dhana potofu kwamba polisi wote wanashirikiana na magenge ya uhalifu, akisema, “Kwa sababu ya majaribio ya hapo awali, watu waliona umuhimu wa polisi, na ni muhimu kwa wananchi kutambua kwamba polisi wanatimiza majukumu yao ipasavyo.”
Awaonya wanaoendeleza Kampeni za ‘Samia Must Go’
Nchimbi alipinga kampeni inayotaka Rais Samia Suluhu Hassan aondolewe madarakani kwa kusema, “Uchaguzi umewekwa kwa miaka mitano, na wale wanaoshindwa na utendaji wa Rais wanapaswa kusubiri uchaguzi ujao badala ya kutoa matamko yasiyokubalika.”
Pia aliwashutumu wale wanaosema kuwa viongozi wa CHADEMA, kama Mbowe na Mnyika, wanahusika na vitendo vya uhalifu.
“Tunapokea taarifa nyingi, nilikuwa nasoma mitandao juzi na jana nimesoma maneno mazitomazito, kuna taarifa kama tatu nimesoma zinasema ndani ya CHADEMA kuna mgogoro mkubwa, kwahiyo Mbowe nae ni Mtuhumiwa wa mauaji haya, nilikuwa na Mbowe kwenye sherehe moja wakati tunaongea na Ndugu Kibao kutekwa na Mimi Walimu wangu wa saikolojia walinifundisha vizuri wakati Mbowe akiniambia kuhusu kutekwa kwa kibao nilikuwa namuangalia machoni kujua huyu anasema uongo, nikagundua anamaanisha, kwahiyo Mimi Mtu akiniambia Mbowe anahusika na utekaji nitamwambia sio kweli kwasababu nimeona akiongea na dhamira yangu inaniambia sioni Mtekaji hapa” alisema Nchimbi na kuongeza
“Mwingine nimemsikia Mwanaharakati Uhuru sijui (Musiba) anasema Mtu wa kwanza anayetakiwa kuhojiwa ni Mnyika kwasababu ndio alikuwa wa kwanza kutoa taarifa, sasa Watu wasitoe taarifa kama Watu wametekwa?, Mnyika yule hata akiona panya anakimbia, kweli Mnyika anaweza kupanga mauaji?, maana kuna Mtu ukitaka kumsingizia tafuta cha kumsingizia lakini Mnyika masikini
Nchimbi alihitimisha kwa kusisitiza kuwa CCM itaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama na kutaka uchunguzi wa kina kuhusu matukio haya, akimpongeza Rais kwa kauli yake ya kuhakikisha uchunguzi wa kweli na kina unafanyika.