Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa iliyokutana jana Septemba 7,2022, imetoa maelekezo sita kwa serikali, kuhusu malalamiko ya utitiri wa kodi hususani za miamala ya simu na ya kibenki,ikiwemo kutazama hali halisi ya maisha na kuchukua hatua stahiki kuhusu utozaji wake wa Kodi
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema maelekezo hayo yaliyotolewa kwa serikali yamezingatia ibara ya 20 (b) ya ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025.
“Naomba kuinukuu, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa gharama nafuu kwa kupanua wigo wa matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za kifedha, ili kuongeza huduma jumuishi za fedha nchini, kuchochea uwekezaji wa ndani na kukidhi mahitaji halisi ya wananchi hususan wa kipato cha chini na waishio vijijini.” Amesema Shaka.
Maelekezo hayo ya Kamati Kuu yamekuja ikiwa tozo za miamala ya simu ilianza kupigiwa kelele tangu ilipoanza kutumika mwaka jana, tozo kwenye miamala ya kibenki imeibua upya hisia za malalamiko kuhusu mzigo wa tozo kwa wananchi.
Shaka amesema licha ya miradi mbalimbali ya maendeleo kutekelezwa kwa fedha za tozo na kuwawekea wananchi mazingira mazuri ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025, lakini serikali haina budi kuwapunguzia wananchi makali ya maisha kwa kupunguza utitiri wa tozo hususani za kieletroniki na kuweka kodi rafiki.
“Serikali imeweza kufanya mambo makubwa katika kipindi kifupi kwa mfano; ujenzi wa vituo vya afya 234 na shule mpya za sekondari 214 na maeneo mengine kadhaa, ambayo yanagusa maisha ya Watanzania ya kila siku.
“ Hata hivyo baada ya kutafakari na kujadiliana na kubishana vikali, serikali haina budi kufuata maelekezo na siku si nyingi mtapata taarifa ya hatua zilizochukuliwa baada ya maelekezo haya,”
Shaka amewataka wasaidizi wa Rais Samia washuke chini kwa wananchi ili kusikiliza shida zao sambamba na kujua hali halisi ya maisha yao.
“Wasaidizi wa Rais washuke chini kwenda kusikiliza kero za wananchi, tumefanya ziara mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita na Mwanza, kuna changamoto lukuku ambazo si lazima Rais ndio ashuke chini kuzishughulikia, wakijipanga vizuri changamoto hizo zinatatuliwa,” amesema.