Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amekemea wanachama wa chama hicho wanaotolea macho Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na kuwataka kuelekeza nguvu zao katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho utakaofanyika mwaka huu.
Chongolo amesema kumezuka tabia ya baadhi ya wanachama kufikiria zaidi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kutaka nafasi za ubunge na udiwani na kusema tabia hiyo inazorotesha shughuli za chama hicho.
“Mwanasiasa mzuri ni yule anayehangaika siku ikifika, anahangaika na jambo wakati muafaka, anahangaika na uchaguzi huu wa ndani, acheni kupanga safu, acheni kutengeneza watu,” alisema Chongolo.
Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kila mwana CCM ana haki ya kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho na kusisitiza hakuna mwanachama mwenye hati miliki wa nafasi yoyote.
“Ni haki ya kila mmoja kujitokeza na kutimiza wajibu wa kikatiba kugombea nafasi yoyote, usitishwe, usiogopeshwe, usibabaishwe, jipime usiogope chochote sote tuna haki sawa katika uchaguzi hakuna aliye zaidi ya mwingine,” alisema.
Alisema kwa kipindi kifupi akiwa katika mkutano huo amepokea meseji zaidi ya 800 za watu kufanyiana fitina, jambo alilosema ni nongwa na halisaidii.
“Tumepita mwaka 2010, tumeenda 2015, leo unakuja kumuhukumu mtu kwa mambo ya 2010, huo ni uchawiuchawi, acheni nongwa, acheni watu watumie haki zao za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi kugombea nafasi mbalimbali,” alisisitiza.
Chongolo aliwataka wanachama wa CCM wakiwemo wanawake na vijana kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.