Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo waache kutumia lugha za kejeli na matusi wanapowakosoa viongozi wa Serikali na chama tawala wakiwa kwenye mikutano ya hadhara.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto amesema hawatakubali kuona wanasiasa wanatumia majukwaa kueleza uongo na kupotosha umma kwa makusudi ili Serikali ichukiwe.
Kauli hiyo ya CCM inatokana na mikutano miwili ya hadhara iliyofanywa na chama cha ACT-Wazalendo Februari 26, huko Nungwi Unguja na Machi 4 Tibirinzi Pemba mwaka huu, ambapo viongozi wake waliibua masuala mbalimbali waliyodai ndiyo chanzo cha umasikini wa Zanzibar na viongozi wameshindwa kuyatatua.
Mbeto amesema CCM ipo tayari kukosolewa na kuelezwa kasoro zilizopo, lakini kwa njia ya kistaarabu bila kutumia kauli za kejeli na matusi kama wanavyofanya baadhi ya viongozi wa ACT-Wazalendo.
Hata hivyo Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma wa ACT Wazalendo, Salim Bimani alisema chama kimekosoa kwenye mikutano ya hadhara na wamejenga hoja kwa wahusika, hivyo watoke hadharani wajibu hoja.
“Sisi tunathamini utawala bora na utawala wa sheria, tunaamini Zanzibar moja, yenye mamlaka kamili, tunataka vyombo husika vionyeshe kasoro tulizotaja.” na kuongeza kuwa
“Lakini hatujakashifu, pengine kuna jambo limemuuma mtu sisi tumezungumza ishu na ishu ndio siasa, tunaheshimu taratibu zote za kisiasa,” alisema Bimani.
Kuhusu sakata la umiliki wa kampuni ya usafirishaji Uwanja wa ndege wa Zanzibar (Dnata) kuchukua asilimia zote na kuwaacha wazawa Mbeto amesema sakata hilo wanaliachia vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake.
Alisema kupitia kampuni hiyo tayari kuna ajira zaidi ya 375, sawa na asilimia 70 zimetolewa.
Kuhusu mamlaka kamili inayodaiwa viongozi wa ACT-Wazalendo, Mbeto alisema Zanzibar inatakiwa ijisimamie. Alisema nchi kuwa na mamlaka kamili sio njia ya kukuza uchumi, kwani yapo baadhi ya mataifa, ikiwemo Hongkong, Dubai na Scotland hazina mamlaka kamili, lakini uchumi wao upo juu duniani.
Akizungumzia ukosefu wa chakula, Mbeto alisema Zanzibar kilo moja ya mchele wa pembe inauzwa Sh2,000, huku kiroba cha kilo 25 kikiuzwa kwa Sh45,000, akidai hakuna ukosefu wa chakula maana kwa mwezi inatumia tani 11, lakini mpaka sasa kuna hifadhi ya tani 50 za mchele.
Alisema ndani ya miaka miwili Serikali imetangaza ajira zaidi ya 2,900 katika sekta za elimu na afya, huku kukiwa na ajira zisizo za moja kwa moja na nyingine katika sekta binafsi, hivyo kufikia mwaka 2025 ajira zilizotolewa katika ilani ya CCM (Zanzibar) zaidi ya 300,000 zitakuwa zimefikiwa.
Mbeto alisema Serikali kupitia mfuko wa hazina imetoa shilingi bilioni 16.8 kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali wadogo na tayari vikundi 2,200 vimeshapewa mkopo huo na walionufaika si makada wa CCM pekee kama ilivyoelezwa.