Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amezitaka kamati za ulinzi na usalama za mikoa kutumia hekina na busara kutatua migogoro ya ardhi iliyoanza kushika kasi maeneo mbalimbali hususani baina ya wananchi na kambi za majeshi.
Jenerali Mabeyo alisema hayo juzi mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya kuaga vikosi vya ulinzi na usalama, pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Morogoro.
Alisema maeneo mengi ya kambi za jeshi hayana hati miliki, hivyo wananchi wamekuwa wakitumia mwanya huo kuvamia na baadaye kudai ni yao.
“Inashangaza kuona maeneo mengi unakuta jeshi linamiliki kwa muda mrefu, baadaye wananchi wanasema ni maeneo yao,” alisema Jenerali Mabeyo na kusisitiza kamati za ulinzi na usalama za mikoa kuitatua kwa hekima na busara.
Alitoa mfano wa eneo la Bwalo la Umwema lililopo katika Manispaa ya Morogoro ambalo amepata taarifa kuwa lina mgogoro huku akiamini ni mali ya jeshi.
“Eneo la Bwalo la Umwema nalifahamu tangu mwaka 1970 wakati nikiwa na cheo kidogo, tulilitumia kwa ajili ya michezo ya majeshi, sasa hivi naambiwa kuna mgogoro,” alisema Mabeyo.
Akizungumzia hali ya usalama nchini, Mabeyo alisema nchi ipo salama, hakuna matukio yoyote ya kutishia amani ya nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi mkoa huo alisema mgogoro wa Bwalo la Umwema umeshaanza kushughulikiwa.
Mabeyo anatarajiwa kustaafu utumishi wa umma mwishoni mwa mwezi huu.