CHADEMA na safari ya maridhiano nchini Tanzania

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema uamuzi wake wa kuzungumza na Chama Cha Mapinduzi (CCM) umebarikiwa vikao vya kikatiba vya chama hicho, hivyo hakitarajii kupoteza wafuasi kwa hilo.

Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na maoni tofauti kutoka kwa baadhi ya wanachama na wapenzi wa chama hicho wakihoji sababu ya chama hicho kufanya mazungumzo na CCM wakiongozwa na Rais Samia Ikulu ya Chamwino Dodoma Mei 21.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Mei 23, 2022, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema uamuzi wa kushiriki mazungumzo hayo umebarikiwa na vikao vyote vya kikatiba vya Chadema na hakitarajii kupiteza wafuasi kutokana na hilo.

Kuhusu ajenda ya Katiba Mpya, Mnyika amesema wamependekeza hatua za kupitiwa, miundo ya vyombo vinavyohitajika ili kuharakisha mchakato na muda inayopaswa kukamilika kabla ya uchaguzi wa 2025.

“Tunaamini hii ni nyenzo ya kupeleka taifa mbele tumependekeza namna ya kukwamua na hatua za kupitiwa, miundo ya vyombo inayohitajika ili kuharakisha huku kukiwa na maridhiano na tumependekeza ratiba ya muda wa kuikamilisha katiba kabla ya uchaguzi wa 2025,” amesema.

Ajenda nyingine, aliyotaja ni kushughulikiwa kwa madhara yaliyotokana na ukiukwaji wa haki uliofanywa katika kipindi cha miaka sita ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano.

Ili kufanikisha hilo, Mnyika amesema katika mazungumzo hayo ya awali, wamewasilisha mapendekezo 10 ikiwemo kuundwa kwa tume ya ukweli na upatanishi na kushugjulikiwa kwa madhara yatokayao na uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na uchaguzi Mkuu 2020.

Mengine ni uhuru wa vyama vya siasa kufanya shughulí zake, kufutwa kesi zenye muelekeo wa kisiasa na kuachiwa wafungwa wa kisiasa, kadhalika kufutwa sheria kandamizi.

Pia, kushughulikia watu walioshambuliwa au kupotea kuhusu siasa, hakikisho la usalama kwa wakimbizi wa kisiasa, kuondolewa bungeni kwa waliokuwa wanachama 19 wa Chadema na kushughulikia masuala yaliyowakumba viongozi kutokana na ukandamizwaji wa demokrasia.

Katika hatua nyingine, Mnyika amesisitiza msimamo wa kutoshiriki kutoa maoni katika kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kufafanua kuwa njia ya mazungumzo wanayofanya wameona ndiyo sahihi itakayoponya majeraha yote.

“Msimamo wetu kuhusu mchakato wa kikosi kazi haujabadilika,” amesema Mnyika.

Aidha, Katibu Mkuu huyo amezungimzia mgogoro wa chama cha NCCR Mageuzi na kueleza kuwa umeondikizwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na imefanya hivyo kwa takribani miaka sita ya utawala wa awamu ya tano.

“Katika kipindi cha miaka sita ya awamu ya tano Ofisi ya Msajili ilipandikiza migogoro na kubadilisha kwa njia haramu uongozi wa vyama vya siasa vitano, sisi bado tunamtamgua James Mbatiakuwa ndiye Mwenyekii wa NCCR Mageuzi,” amesema.

Amezitaka mamlaka zinazoisimamia ofisi hiyo kuimulika vyema na kuichukulia hatua zinazostahili.