Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kilitangaza awamu nyingine ya maandamano yenye utofauti na awamu ya kwanza ya maandamano iliyomalizika hivi karibuni.
Akitangaza Maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho wakati akisoma Azimio la Mtwara akiwa Mkoani Mtwara jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema maandamano hayo ya awamu ya pili yanakwenda kwa jina la”Wiki ya Maandamano” ambayo itafanyika katika Makao Makuu ya Mikoa yote ya Tanzania lengo likiwa lile lile la kuishinikiza Serikali ipunguze gharama za maisha kwa kuja na mpango wa dharula lakini pia kupinga miswada ya sheria tata ya uchaguzi ambayo sasa inayosubiri kusainiwa na rais.
Azimio hili limekuja baada ya maandamano makubwa ya Majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha na hivyo baada ya kuona Serikali haijachukua hatua yeyote katika madai yao sasa wanaingia katika hatua ya pili ambapo maandamano hayo yataanza April 22 hadi April 30, 2024.
“Kwakuwa tulitoa wito kwa Serikali kuleta mpango mkakati wa kupunguza gharama za maisha na wameshindwa, Kamati Kuu imejiridhisha kwamba CCM haina mbinu, utashi wala dhamira ya kupunguza gharama za maisha ya Wananchi, kwahiyo sisi kama Chama pamoja na kuwa hatupo Serikalini, tuna uwezo wa kufikiri, kubuni na kutafiti, kwahiyo Kamati Kuu imeielekeza Kamati ya Wataalamu wa Chama kuandaa mpango wa Taifa wa kunusuru Wananchi na gharama za maisha, kupunguza bei za bidhaa na huduma muhimu na mzigo mkubwa wa maisha magumu unaowakabili Wananchi”- amesema Mbowe wakati akisoma Azimio hilo la pamoja
Maamuzi hayo ya wiki ya maandamano yanayofanyika na Chadema ni sehemu ya azimio lilioandaliwa na kamati kuu ya chama hicho iliyokutana kwa kuanzia Machi 4 hadi Machi 6 mkoani Mtwara.
Hata hivyo kumekuwa na mitazamo tofauti ya wa wagau juu ya mwendeleo wa maandamano hayo ambapo wapo wanaokubalina moja kwa moja na adhma ya CHADEMA kwenye maandamano hayo na wapo wanaokosoa kwa kukosa imani ya kwamba hawadhani kama Serikali itachukulia maanani matakwa ya CHADEMA.
Lakini wanakiri kwamba maandamano yaliyofanyika katika majiji manne yameonyesha ukomavu wa kisiasa ambao hapo mwanzo haukuwepo kutokana na kuminywa kwa uhuru wa wanasiasa katika kufanya shughuli zao licha ya kuwa ni haki yao.