Chadema wapinga wananchi wa Ngorongoro kuondolewa kwenye ardhi yao

Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kimepinga amri ya Serikali iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali namba 673 la tarehe 02 Agosti, 2024, ambapo kwa mujibu wa chapisho hilo  imewaondoa wananchi wote wa Tarafa ya Ngorongoro kwenye ardhi yao kwa kufuta Kata, Vijiji na Vitongoji vyote vya Tarafa hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa leo na Chadema, imeeleza kuwa kabla ya amri hiyo Serikali ilisitisha huduma za kijamii kwa wananchi hao kama kuondoa huduma za afya, elimu, na kusimamisha miradi yote ya maendeleo katika tarafa ya Ngorongoro.

Aidha Chadema imesema Serikali imehamisha taarifa wapiga kutoka kwenye daftari la kudumu  la wapiga kura kutoka tarafa ya Ngorongoro na kuzipeleka Msomera bila ridhaa ya wananchi.

Tamko la Chadema limekuja ikiwa leo ni siku ya tatu tangu maandamano ya amani ya Wamaasai wa Ngorongoro yaanze wakishinikiza Serikali kuwarudishia huduma za kijamii zilizoondolewa katika tarafa hiyo pamoja na kuondolewa kwa vijiji vyao kwenye haki ya kupiga kura.

 Chadema wanaitaka Serikali, Mosi kurudi mezani kufanya mazungumzo na wananchi hao kupata ufumbuzi wa kudumu, pili Serikali ifute amri ya kuwataka jamii hiyo iondoke Ngorongoro, kwani kuendelea kwake kunaweza kusababisha maafa na kuhatarisha amani ya nchi.

Pamoja na hayo pia imeitaka Tume ya Uchaguzi kuzingatia sheria inayoitaka tume hiyo kutokubali kupokea amri ya mtu au taasisi yoyote na irudishe majina ya wapiga kura walioandikishwa kwenye tarafa ya Ngorongoro.