Chadema yabaini kikosi kazi kinachohusika na utekaji nchini Tanzania, Polisi Kanda Maalum Dar yaongoza genge hilo.

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania chama cha Chadema, kimesema utekaji unaoendelea nchini humo kwa zaidi ya asilimia 60 unafanywa na Jeshi la Polisi kupitia kikosi kazi maalum kilichoandaliwa kwa kazi hiyo.

Chadema imetoa kauli hiyo leo Agosti 22,2024 chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, ambaye amewaeleza wanahabari kwamba kiliona kuna haja ya wao kufanya uchunguzi wao kuhusu matukio hayo ili kubaini ukweli uliojificha.

Hivi karibuni Chama cha Wanasheria wa Tanganyika kilitoa ripoti yake inayoonyesha zaidi ya watu 80 wametekwa na hadi sasa hawajulikani walipo.

Katika uchunguzi uliofanywa na Chadema wamebaini kuwa utekaji kwa zaidi ya asilimia 60 unafanywa na mamlaka katika Kanda Maalum ya Polisi Dar es salaam ambako kuna kikosi kazi maalum kinachoongoza genge la watekaji.

“Kama Chama tumechunguza kutoka vyanzo vyetu vya ndani na vingine vya ndani ya Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, nitaeleza kwa kifupi tulichogundua na tunaowaonyooshea vidole ili Polisi na hao wengine watusute watuambie Mbowe mnasema uongo, uchunguzi wetu unatupeleka wapi? moja kuna kitu kwenye Kanda Maalum ya Dar es saalam kinaitwa Task Force ya Ulinzi na Usalama, Task Force hii iliundwa ikishirikisha Wadau kutoka Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na hata JWTZ, katika hatua ya baadaye Jeshi la Wananchi liliondoka katika oparesheni hii, na Task Force hii ilipoundwa kwa mara ya kwanza iliundwa kama Kikosi maalum cha kupambana na wizi ambacho kinasimamiwa na ZCO ambaye sasa hivi anayeongoza Ofisi hiyo anaitwa ASP Faustin Mafwele huyu ndio Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es salaam ambaye anasimamia Kikosi hiki” amesema Mbowe kwenye taarifa yake.

Wimbi la utekaji linaendelea kushamiri huku likiacha vilio na maumivu makali kwa familia, wapo waliopatikana na wapo ambao hadi sasa hawajulikani walipo.

Wanaharakati na vyama vya upinzani nchini Tanzania wananyooshea kidole Serikali chini ya vyombo vyake vya ulinzi na usalama wakidai wanahusika na dhuluma hiyo.

“Kwa taarifa tulizonazo kwa mwaka huu na sehemu ya mwaka jana, wapo Watanzania zaidi ya 200 hawajulikani walipo na mambo haya ni mwendelezo wa maelekezo ya Viongozi wa Serikali ambao huko nyuma walipaswa kusema shughulikeni nao” amesema Mbowe.

Serikali ya Tanzania ilinukuliwa ikisema hakuna utekaji nchini, bali watu wanatumia mbinu za utekaji kujiteka.

“Sisi kama Chama tumesema tuyaseme haya kwa sauti ili yasikike zaidi, utekaji huu umeambatana na mauaji, awali waliokuwa wanauawa kienyeji walikuwa wanapelekwa mochwari, wengine kama Sativa walipelekwa pori la Katavi wakaliwe na Fisi kwasababu wanasema Katavi ndio pori lenye Fisi wakali ambao hata mfupa wanautafuna kama biskuti, Mungu hakupenda akamwokoa, Sativa alikamatwa na hicho Kikosi Kazi na Mafwele anajua na kikosi hiki ndicho kimemkamata Soka, Mlay na Mbise”

-Wataka Tume ya Kimahakama kuchunguza utekaji-

Kwa sasa Jeshi la Polisi limepoteza imani kwa raia hali inayofanya kutoaminika kwenye kazi zao.

Chadema wametaka Rais Samia kuunda Tume ya Kimahakama kufatilia na kuchunguza matukio ya utekwaji yaliyotokea na yanayoendelea kutokea na sio kuwap Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi huo.

“Sisi sio Malaika inawezekana tuna makosa tukamateni na mtupeleke Mahakamani tujitetee kwa sheria za Nchi na sio kututeka na kututesa kutulazimisha tukiri makosa ambayo hatuna, tatizo kubwa Jeshi hilihili ambalo ndio Watenda dhambi ndio linajichunguza, tunamtaka Rais Samia atumie Mamlaka yake kwa mujibu wa sheria ya uchunguzi mahususi, aunde Tume ya Kimahakama ya Majaji ichunguze tuhuma zote hizi, iwasikilize Wahanga na Mashuhuda”

“Ni matumaini yangu Kamisheni hii itakayoundwa itaweza kusimamia kweli na haki na iwarejeshee Watu haki na uhuru wao na Rais apige marufuku Task Force ya Vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama, kwasababu Askari hawa wengine wamehusika kwenye utapeli na uhalifu kwa kutumia mwamvuli wa Polisi” 

Pamoja na hayo wamemtaka Rais Samia kufikiria kuondoa sheria inayowapa nguvu Usalama wa aTaifa kukamata watu pindi tu wanapohisi kuna hatari ya usalama wa nchi.

“Rais afikirie tena, mwaka jana ilipitishwa sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 2023 ambapo katika kifungu cha 4(3) kinatoa ruhusa kwa Maofisa wa Usalama Taifa kukamata Watu wanaowadhania wao wanahatarisha usalama wa Nchi, sasa usalama wa Taifa katika Nchi yetu hawana mfumo rasmi wa kukamata, kuhifadhi na kushtaki kama ilivyo kwa Polisi kwa kutumia PGO ndio sababu Watu wakipotelewa Watu wao wanakimbilia Polisi ambako tunajua kuna utaratibu wa kisheria” amesema Mbowe na kuongeza kuwa

“Kumbe leo kuna Mamlaka nyingine ya kiusalama inakamata Watu, hatujui wanawapeleka mahabusu wapi?, zamani Usalama wa Taifa wanamuhitaji Mrema watatumia Polisi, Polisi watamkamata Mrema wao watamfuata kule Polisi kwenda kumuhoji.Sheria hii iliyopitishwa mwaka jana Usalama wa Taifa anaweza kutokea kokote akakudaka popote akapotea na wewe hujui amepelekwa Mahabusu gani na hauna pa kuuliza, tunataka Rais afute kifungu hiki kinachotoa Mamlaka kwa Maafisa Usalama kukamata, nimemtaka Rais kwasababu ndiye mwenye Mamlaka kwakuwa Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama vipo chini yake ”