Chadema yagoma kushiriki mkutano wa msaijili hadi Mbowe aachiwe

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakitashiriki vikao vya majadiliano ya wadau wa vyama vya siasa, vilivyoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi, hadi mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, atakapoachwa huru bila masharti yoyote.

 Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila, ameyasema hayo leo mbele ya wanahabari akitoa maazimio ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho, kilichofanyika Oktoba 10,2021 kwa njia za kidigitali.

“Sisi kama Chadema hatuwezi kwenda kwenye vikao vya msajili, mpaka mwenyekiti wetu aachiwe bila masharti yoyote. Sababu Watanzania, Serikali na dunia inajua kwamba Mbowe sio gaidi amebambikiziwa kesi kwa lengo la kumtesa,” amesema Kigaila.

Kigaila amesema, chama hicho  hakiwezi kushiriki kikao hicho wakati mwenyekiti wake yuko mahabusu, kwa kesi ya kubambikiwa.

“Hatuwezi kwenda kwenye kikao kujadiliana chochote wakati kiongozi wetu yuko ndani, tunataka Serikali ifute mashtaka ya kubumba waliyomtengenezea mwenyekiti wetu atoke, aachwe huru ili kama kuna vikao vya kwenda twende naye,” amesema Kigaila.

Ikumbukwe msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ameitisha kikao kitakachofanyika jijini Dodoma Oktoba 21, kikao abacho kitawakutanisha wadau wa vyama vya siasa, ikiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Simon Sirro lengo kutafuta suluhu ya changamoto zinazokabili shughuli za vyama vya siasa Tanzania.

Mbali na chama cha CHADEMA, vyama vingine vilivyoweka mkazo wa kutohudhuria mkutano huo ni chama cha NCCR Mageuzi, ACT Wazalendo na Chama cha Wananchi(CUF).