Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekosoa na kukataa Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza ghasia za siku ya uchaguzi na zile zilizoendelea baada yake, kikidai kuwa Rais hana uhalali wa kuunda tume hiyo kwa kuwa matukio hayo yametokana na utawala wake.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Novemba 19, 2025, amesema Rais Samia hana mamlaka ya kimaadili wala kisiasa kuunda chombo cha kuchunguza kile chama hicho kinachokitaja kuwa ni uhalifu uliotekelezwa na Serikali yake dhidi ya raia waliokuwa wakidai haki zao za kidemokrasia.
“Haiwezekani mtuhumiwa ajichunguze mwenyewe halafu tutarajie haki. Serikali ya Samia ndiyo iliyoasisi, kuratibu na kutekeleza mauaji, utekaji, mateso, unyanyasaji na ukiukwaji mpana wa haki za binadamu. Wote aliowateua ndani ya tume hiyo waliwahi kuwa watumishi wa Serikali na pia ni wanachama wa chama anachokiongoza,” amesema Heche.
Kauli hiyo ya Chadema imekuja siku moja baada ya Rais Samia kuunda tume inayoundwa na wabobezi wa sheria na wanadiplomasia waliowahi kuitumikia Serikali katika nyadhifa mbalimbali.
Heche amedai kuwa tume hiyo si huru, akisema inalenga kuficha ukweli, kufuta ushahidi na kuendeleza maumivu kwa waathirika. Ameendelea kusisitiza kuundwa kwa Tume Huru ya Kimataifa yenye mamlaka, weledi na uaminifu wa kufanya uchunguzi huru na wa kina.
“Chadema inasisitiza iundwe Tume Huru ya Kimataifa yenye uwezo, weledi, mamlaka na uaminifu wa kuchunguza kwa uhuru na umakini mauaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na utawala wa Samia,” amesema.
Aidha, chama hicho kimetoa wito kwa taasisi za kimataifa zikiwemo Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama (UNSC), Mahakama ya Kimataifa (ICC), tume za haki za binadamu za kikanda na kimataifa pamoja na mataifa rafiki na wadau wa demokrasia, kuchukua hatua za haraka kuishinikiza Serikali kuruhusu uchunguzi huru wa kimataifa.
Tanzania ilikumbwa na ghasia za uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025, ambapo inakadiriwa kuwa mamia ya vijana walipoteza maisha na zaidi ya watu 500 kufikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini.