Chadema yatafakari uamuzi wa Mahakama kesi ya kina Mdee

Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam jana Desemba 14,2023, ilibatilisha uamuzi wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) la kuwavua uanachama wabunge wa Viti Maalum, Halima Mdee na wenzake 18 ambao walituhumiwa kwenda Dodoma kuapishwa bila idhini ya chama hicho

Akitoa uamuzi huo Jaji Cyprian Mkeha amesema kitendo cha wajumbe wa Kamati Kuu kuwa pia wajumbe wa Baraza Kuu na kutoa uamuzi wa rufaa ni kinyume cha kanuni za haki asili.

Wakili wa wabunge hao, Edson Kilatu ameishukuru mahakama kwa kutenda haki huku akisema “yapo baadhi ya maeneo ambayo pengine tulistahili kupata zaidi lakini tumepata pungufu ya kiwango kwa mfano mahakama kusema imebatilisha maamuzi ya baraza kuu lakini imeachia maamuzi ya kamati kuu.

Kwa maana kwamba CHADEMA itatakiwa iende ikazingatie sheria pamoja na taratibu za chama kwenda kuwasikiliza kwenye ngazi ya baraza kuu peke yake. Lakini sisi tunaona ilitakiwa maamuzi kuanzia ya kamati kuu yalitakiwa yaweze kubatillishwa,” amesema.

Kwa upande wa CHADEMA, wakili wa chama hicho, Dickson Matata amesema mahakama imefuta maamuzi ya rufaa ya baraza kuu lakini uamuzi ya kuwafuta uanachama ambayo yalitolewa na kamati kuu ya chama yako pale pale, huku chama hicho kikieleza kuwa kitaitisha upya baraza kuu na kufuata sheria kuwavua uanachama.

Hata hivyo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema, kinautafakari uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kutengua uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho dhidi ya waliokuwa wanachama wake 19 akiwamo Halima Mdee.

 Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ametoa taarifa kwa umma akisema wanautafakari uamuzi ikiwamo kumkumbusha Spika wa Bunge.

“Kwa uamuzi wa kuwafukuza uanachama waliokuwa wanachama wetu 19 uliofanywa na Kamati Kuu ya chama, umeendelea kusimama (upo palepale) na Mahakama imekubaliana taratibu zote za katiba ya Chadema na sheria za nchi zilifuatwa kikamilifu na Kamati Kuu katika kuchukua uamuzi huo,” amesema Mrema.

Mrema amesema uamuzi wa Baraza Kuu kuhusu rufaa umefutwa, hivyo Baraza Kuu linapaswa kukaa upya kusikiliza rufaa hiyo; lakini Kamati Kuu ilishawafukuza uanachama na uamuzi wake jaji upo sahihi.

“Hivyo basi, kwa hatua ya sasa chama kitawasiliana na mawakili wake ili kutafakari hatua za kuchukua ikiwa ni pamoja na kumkumbusha Spika wa Bunge kuhusu utekelezaji wa uamuzi wa Kamati Kuu ya Novemba 27, 2020 kwani Mahakama imethibitisha walifukuzwa uanachama kihalali na taratibu zote zilifuatwa,” amesema Mrema 

Mbali na Mdee, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Esther Matiko na Ester Bulaya; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; Cecilia Pareso, Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara.

Katika orodha hiyo, wamo pia Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.