Chadema yatakiwa kusimamisha shughuli zake kwa siku 14

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezuiwa kwa siku 14 kufanya shughuli zozote zile za kichama na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam.

Zuio hilo linatokana na kesi namba 8323/2025 iliyofunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa na wenzake wawili ambayo imetolewa uamuzi leo na Jaji Hamidu Mwanga.

Uamuzi huo umetolewa huku CHADEMA ikikosa muwakilishi wa kisheria baada ya Wakili wake Jebrah Kambole aliyekuwa akisimamia kesi hiyo kujitoa kabla ya kutolewa uamuzi akidai kutosikilizwa kwa hoja zao.

Hatua ya CHADEMA kuzuiwa kufanya shughuli hizo inatokana na maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la Mawakili wa walalamikaji ya kwamba liwekwe zuio hilo hadi kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa Juni 24, 2025.

Mbali na Mohammed, wengine ni Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu wanaojitambulisha kama wajumbe wa bodi ya wadhamini.

Katika kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanaiomba Mahakama hiyo itamke na kuamuru amri za kutamka kuwa, wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na katiba ya chama hicho.

Wamechukua hatua hiyo na kuomba Mahakama iamuru na kutamka hivyo wakidai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Pia, wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.