Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kimesema hadi sasa hakijui wapi walipo viongozi wao wakuu, wanachama na wanahabari walioshikiliwa na polisi katika maeneo tofauti wakielekea jijini Mbeya kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyopangwa kufanyika leo chini ya mwamvuli wa Baraza la Vijana CHADEMA.
Naibu Katibu Mkuu Bara Benson Kigaila amewaeleza wanahabari kwamba viongozi hao wote wako chini ya mikono ya Polisi lakini Polisi hawataki kuwaonyesha wapi walipo hali inayowapa hofu juu ya usalama wao.
Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu na Freeman Mbowe wanashikiliwa na Jeshi la Polisi tangu usiku wa kuamkia leo kwa kile walichodaiwa kuhusika kuandaa maandamano ya vijana kwenye maadhimisho ya Siku ya vijana duniani hii leo.
Kadhalika, Jeshi hilo lilidaiwa kuwashikilia na kisha kuwaachia kwa kuwalazimisha vijana wa chama hicho kurejea mikoa wanayotokea ili wasishiriki maadhimisho hayo waliyoyapanga mkoani Mbeya, kusini mwa Tanzania.
Siku ya jana, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kuwa vijana hao wa Chadema walipanga maandamano ambayo yalikuwa yana viashiria vya kuvunja amani.
Katika taarifa iliyotolewa na jeshi hilo ilisema kuwa kiongozi mmoja wa vijana wa chama hicho alikuwa akihimiza kuwepo maandamano kama yale yaliyofanyika nchini Kenya yaliyohusisha vijana maarufu Gen Z.