Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimetangaza kuzindua rasmi mikutano yake ya hadhara mnamo Januari 21, 2023 ikiwa ni siku tatu tu tangu mkuu wa nchi hiyo Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.
Maazimio hayo ya CHADEMA yamekuja mara baada ya makubaliano yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana hapo jana ikiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho bwana Freeman Mbowe.
Taarifa iliyotolewa leo Januari 6, 2023 na chama hicho na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje, John Mrema imesema maazimio hayo yanatokana na Kamati kuu iliyoketi Januari 5, mwaka huu.
“Kamati Kuu katika kikao chake cha dharura Januari 5, 2023 ilipokea na kujadili mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano baina ya timu ya Chadema inayoongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na CCM inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Abdulrahman Kinana,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, Januari 21, 2023 itazindua rasmi mikutano ya hadhara kitaifa, itakayofuatiwa na uzinduzi wa mikutano ya hadhara katika kila Makao Makuu ya Kanda na baadaye ngazi nyingine za chama hicho.
Hata hivyo, ngazi zote za chama hicho zimeagizwa kuendelea na maandalizi ya mikutano ya hadhara.
Kamati Kuu ya Chadema imeazimia pia kuendelea kwa mazungumzo ya maridhiano kati yake na CCM yanayoendelea kwa kile ilichokieleza kuwa imeridhishwa nayo.
Itakumbukwa kuwa Rais Samia alitangaza uamuzi huo, Januari 3, 2023 alipokutana na viongozi wa vyama vya siasa Ikuluna ambapo alisema: “Uwepo wangu mbele yenu ni kuja kutoa ruhusa kwamba lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoshwa”.