Chama tawala cha DRC kimemtaka Kabila aache kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo

Chama tawala cha Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Félix Tshisekedi, kimemjia juu aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, kikimtaka aache kuingilia masuala ya ndani ya taifa hilo na kumtuhumu kuwa si raia halali wa Kongo bali ni raia wa Rwanda.

Katika hotuba yake jana Jumapili, Katibu Mkuu wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), Augustin Kabuya, alimtuhumu Kabila kwa kuhusika na kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda na kudai kuwa Kabila “aliletwa kwa nguvu kututawala” na kwamba hana mamlaka tena ya kutoa mafunzo kuhusu demokrasia.

“Kabila si Mkongo. Awaache Wakongo wajishughulishe na matatizo yao. Yeye ni raia wa Rwanda ambaye utawala wake ulitungwa na kuingizwa kwetu kwa lazima,” alisema Kabuya katika hafla ya chama iliyofanyika mjini Kinshasa.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Kabila kutoa hotuba yake ya kwanza kwa wananchi tangu aondoke madarakani mwaka 2019, ambapo alilalamikia kile alichokiita “vitendo vya kiholela” dhidi yake. Hotuba hiyo ilitolewa siku moja baada ya Bunge la Seneti kupiga kura kuondoa kinga yake ya kibunge, hatua inayowezesha afikishwe mahakamani kwa tuhuma za usaliti kwa kuhusishwa na waasi wa M23.

Kabila, ambaye sasa ni seneta wa maisha kutokana na hadhi yake ya zamani ya urais, ametangaza nia ya kuzuru mji wa Goma ulioko mashariki mwa Congo, eneo linalokumbwa na migogoro mikubwa ya kiusalama na ambalo limetekwa na waasi wa M23 mapema mwaka huu kupitia mashambulizi ya ghafla.

Mwezi Aprili, Wizara ya Sheria ilipeleka suala la Kabila kwenye mahakama za kijeshi, huku Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Jeshi akiitaka Seneti iondoe kinga yake ya kibunge. Seneti iliyodhibitiwa na muungano wa Tshisekedi ilipitisha ombi hilo kwa kura nyingi.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa katiba wamehoji uhalali wa mchakato huo, wakisema huenda ulikiuka taratibu za kisheria. Licha ya hayo, hatua hiyo imeonekana kama sehemu ya juhudi za Rais Tshisekedi kumaliza mzozo wa muda mrefu mashariki mwa nchi hiyo, huku akiendelea na mashauriano ya kidiplomasia.

Rais Tshisekedi hivi karibuni amefungua mlango wa mazungumzo na Marekani, akiahidi kuwapa ufikiaji wa madini adimu ya DRC kwa masharti ya kupata msaada wa Washington katika mazungumzo na Rwanda ili kukomesha mzozo uliodumu kwa zaidi ya miongo mitatu.