Watu watano wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa baada ya basi la Tanzanite kupinduka katika kijiji cha Mbwasa wilayani Manyoni mkoani Singida.
Ajali hiyo imetokea jana Jumatano Agosti 17, 2022 ambapo basi hilo lilikuwa linatoka Mwanza kwenda jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa amesema kuwa ajali hiyo ilitokea wakati basi hilo lilipokuwa likishuka kwenye mlima Saranda na kusababisha vifo vya watu watano akiwamo Diwani wa Iramba Mwinjuka Mkumbo (40).
Kamanda Mutabihirwa amesema majeruhi 15 walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General Dodoma) kwa ajili ya matibabu ambapo baada ya uchunguzi na kupata matibabu, abiria kumi waliruhusiwa.
Amewataja waliopoteza maisha ni Diwani wa Iramba Mwinjuka Mkumbo (40) ambaye alifia hospitalini wakati akipatiwa matibabu, mtoto Alicia Flagence (01) na wengine watatu ambao miili yao haijatambuliwa hadi sasa.
“Hadi sasa majeruhi Sharifati Mwipi (32), Rudia Daniel maarufu Kudia (59), Saidi Mbwana (39) na Adul Ramadhan (32) wanaendelea na matibabu katika hospitali ya rufaa ya Dodoma na hali zao zinaendelea kuimarika,” amesema Mutabihirwa.
Hata hivyo, amesema majeruhi mwingine Ngisa Sita (26), alipewa rufaa ya kwenda hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na hali yake kuhitaji madaktari bingwa.
Kuhusu dereva wa basi hilo, alisema baada ya kutokea kwa ajali hiyo, dereva Abdul alitoroka na kukimbilia kusikojulikana na kwamba wanaendelea kumsaka ili kumfikisha katika vyombo vya sheria.
Chanzo cha ajali hiyo kimetajwa ni mwendokasi wa dereva wa basi hilo uliosababisha ashindwe kulimudu basi kisha kupoteza mwelekeo na kuacha njia kisha kupinduka.