Kamati ya kufuatilia mwenendo wa matokeo ya mitihani ya mafunzo ya uansheria kwa vitendo (LST), imeanisha changamoto nane ikisema ni miongoni mwa vikwazo katika kupata wanafunzi bora wanaosomea fani ya sheria nchini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Harrison Mwakyembe amesema changamoto hizo pia zimelalamikiwa na LST pamoja na wadau mbalimbali wa sheria.
Dk Mwakyembe ameeleza hayo jana Jumapili Novemba 20, 2022 wakati akisoma muhtsari wa taarifa ya kamati hiyo kufuatilia chanzo cha wanafunzi wengi kufeli katika mitihani ya mafunzo katika taasisi ya LST.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo, wajumbe wa kamati hiyo pamoja viongozi waandamizi wa wizara hiyo.
Kamati hiyo yenye wajumbe saba iliteuliwa Oktoba 12, mwaka huu na Dk Ndumbaro na kufanya kazi kwa siku 30 kufuatilia sakata la kufeli kwa wanafunzi wengi wa taasisi hiyo.
Kuundwa kwa kamati hiyo kulitokana na kuibuka kwa taarifa zilizoonyesha matokeo ya awamu (Cohort) ya 35 ya wanafunzi wa taasisi hiyo, kuonyesha kati ya wanafunzi 633 waliofanya mtihani huo, ni 26 ndio waliofaulu kwa awamu ya kwanza.
Katika matokeo hayo, wanafunzi 265 walifeli (discontinue) na wengine 242 walitakiwa kurudia mtihani (supplementary).
Dk Mwakyembe amesema udahili wa wanafunzi wengi kupita uwezo katika vyuo vinavyofundisha sheria na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo unasababisha uwiano mbaya kati walimu na wanafunzi na kuathiri ufundishaji na usimamizi.
Pia Dk Mwakyembe ambaye ni waziri wa zamani wa Katiba na Sheria amesema kumekuwa na uhuria usio kuwa na tija kwa kila chuo kuwa na uhuru wa kupanga muda wa kukamilisha shahada ya sheria kati ya miaka mitatu au minne.
“Pia uwezo mdogo wa wanafunzi wengi wanaoruhusiwa kusoma sheria na baadaye kujiunga na LST katika kumudu lugha ya kufundishia ya kiingereza.Tatizo hili lina athari kubwa katika uelewa wa masomo ya kujieleza,” amesema Dk Mwakyembe.
Mbali na hilo, amesema uamuzi wa Tume ya Vyuo Vikuu kushusha vigezo vya ufaulu katika mitihani ya kidato cha sita kutoka alama nane (B mbili kwa masomo mawili hadi alama nne ( D mbili kwa masomo mawili kulikowezessha vijana wasiokuwa na uwezo kusoma masomo ya sheria.
Ameongeza kuwa utatuzi wa changamoto hizo upo kisera na kimfumo na kwamba mfumo wa bora wa elimu ya sheria unasimamamiwa na ule uanasheria kwa vitendo unasimamiwa na Baraza la Elimu ya Sheria nchini (CLE).
Amesema kamati inashauri kufufuliwa kwa CLE na kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ikiwemo kukaa chini na TCU kupandisha vigezo vya ufaulu wa mitihani ya kidato cha sita na nne kwa wanaotaka kusomea sheria vyuo vikuu.
“Kuanzisha mtihani maalumu wa kuingia LST kama ilivyo kwa wenzetu wa Afrika Mashariki ambao utasimamiwa na CLE, “ amesema Dk Mwakyembe.