Dar kurejeshewa hadhi yake ya kuwa jiji

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ameelekeza mchakato wa uanzishaji wa Mamlaka ya Usimamizi  wa Jiji la Dar es salaam uanze mara moja ili kuratibu maendeleo yote yanayofanyika kwenye Halmashauri za Mkoa wa Dar es salaam.

Mchengerwa ameyasema hayo leo  katika hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara katika halmashauri tano za Mkoa wa Dar es salaam kwenye viwanja vya Mwengeyanga Manispaa ya Temeke.

Amesema Mkoa wa Dar es salaam unatakiwa kuwa Kioo cha nchi  na wageni wote wanapokuja hapa wanatakiwa kuona sura ya Tanzania hivyo inapaswa kuwa na chombo kinachoratibu maendeleo yake na kuhakikisha kuwa mipango yote ya maendeleo inayofanyika na inakua na muunganiko.

Ameongeza kuwa kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam awamu ya Pili  (DMDP II) kuna miradi mikubwa inayotekelezwa kama ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara na uendelezaji wa bonde la mto msimbazi hivyo miradi mikubwa kama hiyo kwenye halmashauri inahitaji chombo cha kusimamia.

“Hata majiji makubwa duniani yote yanakuwa na ‘Metropolitan City’ na sio halmashauri zinazojitemea kila moja inapangwa kivyake kunatakiwa kuwa na chombo ambacho kinaunganisha jitihada zinazofanywa kwenye halmashauri zote na kuzitaribu ili Jiji husika liweze kukua kwa viwango vya kimataifa.”

“Nataka hii Dar es salaam iwe ya viwango na ubora na ukuaji wake uratibiwe kwa taratibu maalunu na sio kukua kiholela tu hii itafanya hadhi ya Dar es salaam isikue haraka na kuwa na hadhi ya  kimataifa,”amesema.

Februari 24, 2021, aliyekuwa Rais wakati huo Hayati John Magufuli alitangaza kulivunja jiji la Dar es salaam na kupandisha moja kati ya manispaa zake kuwa jiji. Raisi Magufuli alitangaza uamuzi huo wakati wa uzinduzi wa daraja la juu la Kijazi lililopo Ubungo,hafla iliyohudhuriwa na viongozi waandamizi kadhaa wa Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo ya Tanzania.