Daraja la Tanzanite linalopita juu ya Bahari ya Hindi limekamilika na litaanza kutumiwa na wakazi wa Dar es Salaam kuanzia kesho Februari Mosi 2022.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema daraja hilo linatarajiwa kupunguza msongamano wa magari katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Barack Obama wakati wa kuingia na kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Daraja la zamani la Selander linapitisha zaidi ya magari 45,000 kwa siku, hivyo kukamilika daraja jipya kutasaidia kupunguza idadi ya magari yanayopita katika daraja la zamani la Selander na hivyo kuepusha msongamano wa foleni.
Mbali na foleni, pia litasaidia kukuza sekta ya utalii kwa sababu eneo hilo liko pembeni ya fukwe ya bahari ambapo watu wengi watakuwa wakienda kujivinjari.
Daraja hilo lina urefu wa kilometa 1.03, lina njia nne za magari na njia mbili za watembea kwa miguu na limejengwa pamoja na barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 5.2.
Gharama za ujenzi Daraja la Tanzanite ni takribani shilingi bilioni 243, na limesimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), huku Mkandarasi wa mradi wa huu ni GS Engineering kutoka Korea Kusini, Mhandisi Mshauri ni Kampuni ya Yooshin Engineering kutoka Korea Kusini ikishirikiana na Afrika Consulting ya Tanzania.
Daraja hilo linatarajiwa kudumu kwa muda wa takribani miaka 100 ijayo.