Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dkt Godwin Mollel ni kwamba wanawake 263 wamepoteza maisha kutokana na uzazi katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2021, huku miongoni mwa sababu zikielezwa kuwa ni dawa za ganzi, upasuaji wakati wa kutolewa mtoto tumboni, tatizo la damu kuganda na maambukizi ya bakteria baada ya upasuaji.
Naibu Waziri huyo amesema ufuatiliaji uliofanywa na serikali ya nchi hiyo umebaini kuwa kwa mwaka 2018, vifo vilivyosababishwa na dawa za ganzi na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni ni 53 sawa na asilimia 3.
Amesema mwaka 2019 kulikuwa na vifo 80 yaani asilimia 4.8 mwaka 2020 kulikuwa na vifo 65 sawa na asilimia 4, mwaka 2021 kulikuwa na vifo 65 sawa na asilimia 4.5
“Wizara inashirikiana na vyama vya kitaaluma kutekeleza mkakati kwa kuwajengea uwezo watumishi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi za zahanati, hadi hospitali za taifa katika eneo la utoaji ganzi na upasuaji kwa usalama kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya,” amesema.