DC akiri kupokea tozo za miamala ya simu kwa ajili ya sekta ya afya           

Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Festo Kiswaga amesema wamepokea shilingi bilioni mbili  kutoka serikalini zilizotokana na tozo za miamala ya simu kwa ajili ya sekta za afya na elimu.

Kiswaga aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya kutembelea miradi tofauti iliyotekelezwa na fedha za tozo ikiwemo Shule ya Sekondari Nyawile iliyopo Kata ya Kashishi iliyojengwa vyumba viwili vya madarasa kwa  gharama ya shilingi milioni 25.

Kiswaga alisema fedha za tozo zimefanya kazi kubwa kwenye sekta ya elimu kwani wanafunzi wenyewe wa shule hiyo ni mashahidi walikuwa wakitembea umbali wa kilometa zaidi ya 20 kwenda Shule ya Sekondari Bulige.

Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Msalala, Elikare Zebron  alisema wao walipokea  shilingi milioni 537.5 fedha ambazo zimetokana na tozo za miamala  ambapo sekta ya elimu  walipokea shilingi milioni 37.5.

Zabron alisema shilingi milioni 12.5 zimejenga chumba kimoja cha darasa  katika Shule ya Sekondari ya Chela,  shilingi milioni 25 vyumba viwili vya madarasa Nyawile na Sh milioni 500 ujenzi wa Kituo cha Afya Mwalugulu.

Ofisa Slimu Sekondari kutoka halmashauri hiyo, Seleka Ntobi alisema kuna jumla ya shule 20 za sekondari ambapo vyumba  vya madarasa 72 vimejengwa kwenye shule hizo kutokana na fedha za tozo na zile za Covid-19.

“Changamoto iliyokuwa ikiwakabili  wanafunzi  ni kuwepo msongamano darasani, utoro uliosababishwa na umbali na kutopata chakula cha mchana, hayo yote serikali inaendelea kuyatatua,” alisema.

Makamu mkuu wa shule  hiyo, James Matiku alisema shule ilianzishwa mwaka 2021 ambapo ina jumla ya wanafunzi 266 wa kidato cha kwanza 190 na kidato cha pili ni 76 na sasa ina vyumba tisa vya madarasa.

Chanzo Habari Leo.