Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, linamshikilia dereva wa daladala mkazi wa Kimara Suka Golani Wilaya ya Ubungo, Maarifa Hadith Matala (45) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake Kondakta wa daladala aliyekuwa mkazi wa Kimara Suka Golani Wilaya ya Ubungo, Sharifa Twaha Nyamaishwa (31), kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Agosti 16, 2022 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Jumanne Muliro imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Agosti 16, maeneo ya Kimara Suka.
“Baada ya tukio hilo mtuhumiwa alitoweka. Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa hiyo lilianza upelelezi na ufuatiliaji wa haraka na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Mkoani Lindi alipokuwa amejificha.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa wapenzi hao walikuwa na migogoro inayosababishwa na wivu wa kimapenzi na kupelekea kugombana mara kwa mara, na mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha.
“Uchunguzi wa shauri hili unakamilishwa na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya tuhuma hizo za kikatili uliovuka kiwango” imeeleza taarifa hiyo.