Search
Close this search box.
Africa

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu watatu akiwemo Diwani Kata ya Iganzo, Daniel William kwa tuhuma za kumshambulia kwa kipigo Shadrack Zacharia (25) ndani ya ofisi za Serikali.

Wengine waliokamatwa kwa tuhuma hizo ni Mtendaji wa Mtaa na Mkazi wa Mtaa huo, Erasto Mwankenja na mkazi wa mtaa huo, Henje Mbobo (74).  

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei amesema tukio hilo limetokea Machi 3, 2022 majira ya saa 2 za asubuhi.

Amesema uchunguzi wa awali unaeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni kumtuhumu kijana huyo kuwapiga picha bila idhini yao na kuziba njia ambayo ilikuwa ikitumiwa na wananchi, jambo alilosema halikupaswa kumshambulia kwa kipigo na badala yake wangetumia busara.

”Awali baada ya tukio hilo kuna kipande vya video kilikuwa kimesambaa kwenye mtandaoni kikionyesha jinsi alivyokuwa akishambuliwa  sehemu mbalimbali za mwili wake,” amesema Matei.

Amesema kutokana na tukio hilo, Polisi walianza kufuatilia na walibaini kutokea jijini hapa katika Kata ya Iganzo ndani ya ofisi za Serikali.

‘Tunalaani vikali tukio hilo la kujichukulia sheria mikononi. Kwa sasa watuhumiwa kuendelea na mahojiano na watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa,” amesema.

Comments are closed