Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amelitaka jeshi la Polisi nchini humo kutenda haki pasipo kuonea mtu yeyote, na kwamba yeyote anayevunja sheria achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na sio vinginevyo.
Ameyasema hayo leo Agosti 18 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania Inspekta Jenerali Camillus Wambura katika ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam.
“Watu wanachotaka ni haki, sio kuonewa hicho ndicho Watanzania wanataka, mtu ambaye amevunja sheria kikweli kweli achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria”amesema Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amelipongeza jeshi la polisi kwa kuendelea kuimarisha amani pamoja na ulinzi wa wananchi na mali zao, akisisitiza jeshi kuendelea kuhakikisha utulivu unapatikana wakati wote.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amemuagiza IGP Wambura kuangazia malalamiko yanayotolewa na wananchi kwa jeshi la polisi, na kuwachukulia hatua askari wachache wanaoharibu taswira ya jeshi hilo.