Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema kutokana na umuhimu mkubwa wa mradi wa Bomba la mafuta, wananchi wa Tanzania na Uganda wanapaswa kuwa wazalendo katika mradi huo ikiwemo kulinda bomba hilo litakalojengwa, kulinda mazingira na kutoa taarifa za haraka katika kudhibiti viashiria vyovyote vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa mradi huo.
Dkt. Mpango ameyasema hayo jana tarehe 1 Februari 2022 wakati akimuwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya kutoa maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (Final Investement Decision) ya mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga nchini Tanzania (EACOP).
Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya sherehe vya Kololo vilivyopo Kampala Nchini Uganda, na ameungana na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museven kushuhudia tamko la pamoja la Makampuni wabia wa mradi huo pamoja na mashirika ya petroli ya nchi za Tanzania na Uganda ya kuanza uwekezaji katika mradi huo.
Dkt. Mpango amesema serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Bomba hilo ikiwa tayari imelipa fidia kwa wananchi ambao mradi unapita katika maeneo yao pamoja na kutoa kiasi cha shilingi bilioni 259.96 kwa shirika la maendeleo ya petroli Tanzania (TPDC) kwa ajili ya ushiriki katika mradi huo.
Aidha amewataka maafisa wa forodha kutoka pande zote mbili kuharakisha uingizaji wa vifaa vinavyotumika katika mradi huo pamoja na kuwaasa wahusika wote wa utekelezaji wa mradi huo kuchukua hatua stahiki za kulinda mazingira, kufuata sheria za kazi pamoja na haki za wananchi wa maeneo husika wakati wa utekelezaji wa mradi huo.