Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema hakumbuki siku hata moja ambayo walikua na ratiba ya kula chakula cha mchana wakati alipoongozana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara ya aliyoifanya katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumzia mafanikio ya ziara ya Rais Samia aliyoifanya katika nchi hizo siku chache zilizopita.
“Mimi nilivyoambatana na Rais nimeona kwamba anavyokuwa kwenye ziara hizo anakuwa na ratiba ngumu na anazitekeleza kwa ajili ya manufaa ya Watanzania,
“Ni ziara ngumu, nimeambatana naye hizi siku zote, sikumbuki siku hata moja ambayo tulikuwa hata na ratiba ya lunch (chakula cha mchana) kwa hiyo ni kazi mfululizo, kuamka mapema kulala kwa kuchelewa na mikesha inayoambatana na ukamilishwaji wa masuala yanayohusu masilahi mapana ya nchi” amesema
Awali Dk Mwigulu amebainisha baadhi ya mambo yaliyofanyika kwenye ziara hiyo ya Rais Samia kwenye nchi tatu hasa katika sekta ya Uwekezaji, Fedha na Nishati.
Amesema kuwa ziara hiyo imesaidia kusainiwa mikataba mbalimbali na kuwavutia wawekezaji kuja nchini kuangalia fursa zilizopo.
Dk Mwigulu ambaye aliambatana na Rais Samia kwenye ziara hiyo, amesema kuwa katika ziara hiyo, mikataba sita ya miradi ya mikopo nafuu na misaada ilisainiwa.
Kuhusu wawekezaji, Dk Mwigulu amesema kuwa Baraza la Mawaziri linatarajia kukutana Machi 4 kwa ajili ya kuratibu namna ya kuwapokea wawekezaji ambao wanatarajiwa kuingia nchini ndani ya wiki mbili kuangalia fursa zilizopo.