Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania Dkt. Godwin Mollel
Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania Dkt. Godwin Mollel amesema , asilimia 70 ya Mapato ya vituo vya huduma za Afya vya Serikali pamoja na binafsi vinategemea Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuendesha vituo hivyo.
Amesema, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekuwa ni nguzo muhimu katika uboreshaji wa huduma za Afya Nchini ambapo taasisi binafsi za Afya pamoja na vituo vya huduma za Afya vya Serikali vimeonekana kutoweza kujiendesha bila uwepo wa Mfuko huo kutokana na Watanzania wenye uwezo wa kulipa fedha taslimu kuwa wachache.
Dkt Mollel ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Joseph Khenani katika Bunge la kumi na mbili Mkutano wa kumi na moja kikao cha 41, Jijini Dodoma.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali imefanya maboresho kwa kuongeza idadi ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambapo kwa ngazi ya zahanati imeongeza kutoka aina 254 hadi 451 na kwa ngazi ya vituo vya Afya toka aina 414 hadi 828.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kutoa hamasa kwa viongozi wote ikiwemo Wabunge kuunga mkono Bima ya Afya kwa wote pindi mswada huo utapoletwa Bungeni ili wananchi wanufaike na huduma za afya katika ngazi zote kuanzia zahanati mpaka hospitali ya Taifa bila kikwazo chochote.
Ameendelea kusema, katika kipindi ambacho Wizara inaendelea kufanya maboresho kwenye Bima ya Afya kwa wote, Wizara inaendelea kushirikiana na OR TAMISEMI na Wadau wa CHF kuboresha Bima ya Afya ya CHF ili kukidhi mahitaji ya kupata huduma bora kwa wananchi hasa wenye kipato kwa chini.
Aidha, Dkt. Mollel amemwelekeza Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ndani ya siku tatu hospitali ya Wilaya ya Biharamuro ipate huduma za NHIF ili wananchi wa Wilaya hiyo waanze kunufaika na huduma hiyo.