Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile ameitaka serikali kuondoa malipo kwa vyombo vya moto vinavyovuka Daraja la Nyerere, maarufu Daraja la Kigamboni, na mzigo huo wa deni la NSSSF ubebwe na serikali.
Dkt Ndugulile ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma, akisema kwamba wakazi wa Kigamboni hawana njia mbadala ya kutumia kama ambavyo wakazi wa Msasani, Masaki na wengine wanaotumia Daraja la Tanzanite, hivyo kuwatoza fedha ni kuwaumiza kudhorotesha juhudi zao za kujikwamua kiuchumi.
Amesema ni wakazi wa Kigamboni pekee nchini kote ambao wanalipia gharama ya daraja wakati kuna madaraja mengi yamejengwa kwa fedha za mikopo.
“Wananchi wa Kigamboni hawana mbadala, ili mwananchi wa Kigamboni afike mjini aidha afike feri au apite kwa mguu darajani ama kwa wale ambao wana magari ni lazima alipe tozo.Daladala moja ambayo inavuka pale inachajiwa shilingi 5000 kwa ruti moja kama ruti 10 maana yake anachajiwa 100000”
Aidha Ndugulile ameitaka Serikali itafakari kuondoa tozo katika daraja hilo ili iondowe mzigo kwa wananchi kutokana hali ya maisha ya wakazi wa Kigamboni kuwa ya chini ukilinganisha na wakazi wa Masaki wambao wanapita kwenye daraja la Tanzanite bure.
“Serikali itafakari kuondoa tozo kwenye daraja lile la Kigamboni, Serikali ibebe mzigo wa deni lile la NSSF, ili na wananchi wa Kigamboni nao wapate nafuu” amesema Ngugulile
Daraja la Nyerere lilifunguliwa rasmi Aprili 19, 2016 na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ambalo lilijengwa kwa ushirika kati ya mfuko huo (60%) na serikali (40%).