Dkt. Tulia achaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kundi la Kanda ya Afrika ya Umoja wa Mabunge duniani.

Wajumbe wa Kundi la Kijiografia Kanda ya Afrika la Umoja wa Mabunge Duniani (African Geopolitical Group of IPU) wamemchagua  Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kuwa Mwenyekiti wa Kundi hilo ambapo atahudumu kwa muda wa kipindi cha Mwaka Mmoja.

Aidha kupitia nafasi hiyo atakuwa pia Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya IPU na Kamati ya Uongozi ya Makundi ya Kijiografia.

Nafasi hii ni ya juu kati ya nafasi zinazowakilishwa katika Umoja wa Mabunge Duniani kwa mujibu wa Kanuni za uongozi za Umoja huo.

Maspika mbalimbali kutoka Mabunge ya Afrika yamempongeza Dkt Tulia kwa kushika wadhifa huo mara baada ya kuchaguliwa na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Mwenyekiti huyo mpya.

Vilevile, Dkt Tulia ameahidi kuendeleza dira na dhamira ya Afrika katika ngazi ya Dunia na kuhakikisha usawa na uwajibikaji wa Mabunge ya Afrika unafikiwa kwa ufanisi wa hali ya juu.

Uchaguzi huo umefanyika jana Oktoba 10, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kigali (KCC) Nchini Rwanda wakati wa Mkutano wa 145 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).