Dola dhidi ya Madhabahu: Gwajima katika moto wa kisiasa

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendelea kulizingira Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, huku baadhi ya waumini wa kanisa hilo wakishikiliwa kwa mahojiano, kufuatia agizo la Serikali la kulifunga kanisa hilo kwa madai ya ukiukaji wa sheria.

Tukio hilo limeibua mjadala mpana katika jamii huku baadhi wakilitazama kama suala la kiusalama, wengine wakiliona kama mgongano kati ya dini na siasa.

Asubuhi ya leo, maeneo yanayozunguka kanisa hilo lililopo Ubungo, Dar es Salaam, yameshuhudia ulinzi mkali wa Polisi wakiwa na magari ya washawasha, huku utepe wa njano uliandikwa “eneo la tukio” ukifunga sehemu ya mlango mkuu wa kanisa hilo. 

Takriban askari 20 walionekana wakililinda eneo hilo na kuwazuia waumini waliokuwa wakijaribu kuingia kwa ajili ya ibada.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amethibitisha kuwa baadhi ya waumini wanashikiliwa kwa mahojiano baada ya kukaidi agizo la kufungwa kwa kanisa hilo. “Tulitarajia ushirikiano kutoka kwa viongozi wa dini. Agizo la Serikali ni halali, na yeyote anayepinga lazima afuate utaratibu wa kisheria,” alisema Muliro.

Hatua ya Serikali kulifuta kanisa hilo imekuja siku chache tu baada ya Askofu Gwajima kutoa matamshi mazito akidai kuwepo kwa vitendo vya utekaji nchini Tanzania, akisisitiza kuwa hali hiyo inazidi kuchukua sura ya hatari. 

Katika moja ya ibada zilizopita, Gwajima alisema: “Nimeonyeshwa maono ya giza linalokuja juu ya nchi, watu wanapotea, serikali inapaswa kulinda wananchi wake.”

Kauli hizi ndizo zinazoaminika kuwa chanzo cha taharuki na mwelekeo wa kisiasa uliolalamikiwa na Serikali. Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Waziri Innocent Bashungwa, ilieleza kuwa kuna haja ya uchunguzi wa kina kuhusu taasisi za dini zisizofuata taratibu.

“Kuna utitiri wa uandikishaji wa hizi taasisi, unakuta mtu hajasajili kanisa, anatoa huduma, anaamka anasema ameomba ameoteshwa kwamba sijui kitatokea nini. Kama umeona umeoteshwa kutakuwa kuna hali ambayo siyo nzuri, basi nenda uombe Mwenyezi Mungu aizuie isitokee kwenye taifa letu, lakini siyo kutoa taharuki kwa taifa kwamba jana nimelala, nimeota, mimi ni nabii, kutakuwa na taharuki hii. Sasa mimi nilitegemea huyo huyo kiongozi angeenda aombe Mwenyezi Mungu azuie hilo balaa lisitokee, lakini kiongozi huyo analeta taharuki ya nchi, Watanzania waache kufanya shughuli zao waanze kupaniki, lakini ukifuatilia unakuta hajasajiliwa, ukimgusa anasema serikali inavamia viongozi wa dini, kwahiyo tunaenda kufanya uchambuzi vizuri, tutaleta mbele ya bunge hili, tuwaoneshe wale ambao wanafanya kazi kinyume cha utaratibu ili tutakapowachukulia hatua, Watanzania wajue kuwa siyo mambo ya kisiasa”,- amesema Bashungwa

Kupitia video iliyosambaa usiku wa kuamkia leo, Askofu Gwajima alionekana akizungumza na waumini wake na kuthibitisha kuwa polisi walizingira kanisa lake kuanzia saa tano usiku. “Hii ni zaidi ya dini, hii ni vita dhidi ya haki ya kuabudu,” alisema.

Gwajima, ambaye pia ni Mbunge wa Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), hajatoa kauli rasmi kuhusu hatua za kisheria atazochukua, lakini ameonesha dhamira ya kupinga hatua hiyo akisema “haki itasimama.”

Uchambuzi na hatma ya taasisi za dini

Kauli ya Waziri Bashungwa imeibua mjadala mwingine kuhusu usajili na udhibiti wa taasisi za kidini nchini, ambapo Serikali imesisitiza kuwa zoezi la uchambuzi wa taasisi hizo linaendelea, lengo likiwa ni kuondoa zile zinazokiuka taratibu au kutumia majukwaa ya kidini kwa ajenda zisizo za kiroho.

Wachambuzi wa masuala ya dini na siasa wanasema tukio hili linaweza kuathiri mahusiano ya Serikali na baadhi ya viongozi wa dini, hasa wale wanaochanganya mahubiri na masuala ya kijamii au kisiasa.