Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
DRC yatangaza Serikali mpya yenye Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini humo - Mwanzo TV

DRC yatangaza Serikali mpya yenye Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini humo

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeteua serikali mpya leo Jumatano, na hivyo kumaliza mkwamo wa kisiasa uliodumu kwa takribani  zaidi ya miezi mitano ya msuguano kufuatia kuchaguliwa tena kwa Rais Felix Tshisekedi.

Katika taarifa lililotolewa mapema leo na msemaji wa serikali ya Kongo Tina Salama na kurushwa na televisheni ya taifa RTNC, baraza hilo jipya lina mawaziri 54 ikilinganishwa na 57 katika serikali iliyopita.

Tangazo hilo limekuja chini ya wiki mbili baada ya jeshi la nchi hiyo kusema kuwa limezuia jaribio la mapinduzi lililoshuhudia watu wenye silaha wakishambulia nyumba ya waziri kabla ya kuingia katika eneo la Palais de la Nation ambalo lina ofisi za Tshisekedi katika mji mkuu Kinshasa.

Pia ilikuja wakati wa mapigano mapya mashariki mwa DRC, ambapo jeshi la Kongo linajaribu kurejesha eneo lililotekwa na waasi wa M23 (March 23 Movement) wanaoungwa mkono na Rwanda.

Iliyotangazwa mwendo wa saa 02:00 asubuhi kwa saa za huko (0100 GMT), serikali mpya ilimtaja Guy Kabombo Muadiamvita kama Waziri wa Ulinzi, wadhifa muhimu katika wakati ambapo Kongo inakabiliwa na mzozo mkubwa wa usalama mashariki mwa nchi.

Akiwa madarakani tangu 2019, Tshisekedi alichaguliwa tena katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa Disemba, kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura, lakini jukwaa lake la “Muungano Mtakatifu wa Taifa” bado halikuweza kuunda serikali mara moja.

“Ni muungano wa vyama tofauti, kumekuwa na mijadala…, maridhiano”, alisema Erik Nyindu, mkurugenzi wa mawasiliano wa ofisi ya rais, akifafanua kwa nini uundaji wa serikali umechukua muda.

Rais hatimaye alimtangaza Judith Suminwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kongo na aliyekuwa mkuu wake wa utumishi Vital Kamerhe kuwa Spika wa bunge  na hivyo kusafisha njia ya kuteuliwa serikali.

Kinachosubiriwa kwa sasa ni nini kitakuwa kipaombele kwa serikali hii mpya?