Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson ametangaza mabadiliko ya ratiba ya Bunge akisema ni makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Dk Tulia ametangaza mabadiliko hayo leo akisema ratiba mpya sasa inafanya bajeti kuu ya Serikali kusomwa Juni 14, 2022 badala ya 16 iliyokuwa imepangwa awali na kwamba wabunge wataanza kuchangia bajeti hiyo Juni 16 badala ya juni 20, 2022.
Kutokana na mabadiliko hayo, baadhi ya Wizara zimepunguziwa siku za uwasilishaji wa bajeti zake kutoka siku mbili na sasa wabunge watachangia kwa siku moja tu.
Moja ya Wizara zilizoanza kukumbwa kwenye mabadiliko hayo ni Wizara ya Afya ambayo awali ilikuwa bajeti yake ichangiwe kwa siku mbili na sasa bajeti hiyo imesomwa leo na itapitishwa leo jioni ili kupisha Wizara ya Kilimo kwa kesho.
“Waheshimiwa wabunge, mtakumbuka Mei 13 jioni tulikutana kamati ya uongozi kwa ajili ya kujadiliana na kwenye makubaliano yetu tulifanya marekebisho madogo ya ratiba yetu kutokana na makubaliano tuliyonayo kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili bajeti zetu zisomwe siku moja,” amesema Dk Tulia.
Kwa mujibu wa Dk Tulia, kwa sasa bajeti ya Serikali itasomwa siku ya Jumanne kwa nchi zote tofauti na ilivyozoeleka miaka mingi ambapo husomwa siku ya Alhamisi na kuanza kujadiliwa siku ya Jumatatu inayofuata.
Mwaka huu wabunge watasomewa bajeti hiyo siku ya Jumanne na siku ya Jumatano watapumzika ili kusoma bajeti hiyo na kujiandaa kisha wataanza kuijadili siku inayofuata ambayo ni Alhamisi.