Kesi hiyo ambayo ilianza kusikilizwa majira ya saa tatu asubuhi mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Lissu aliendelea na zoezi la kumhoji kwa kina shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka, akichambua maelezo yake ya polisi dhidi ya ushahidi alioutoa mahakamani wiki iliyopita.
Kabla ya mahojiano kuanza, Mahakama ilitoa uamuzi muhimu kuhusu pingamizi lililokuwa limewasilishwa na upande wa Jamhuri wiki iliyopita.
Mnamo Ijumaa, Oktoba 10, 2025, mawakili wa Serikali waliwasilisha pingamizi dhidi ya ombi la Lissu la kutaka kielelezo kinachojulikana kama DE1 (maelezo ya maandishi ya shahidi Kaaya aliyoyatoa akiwa kituo cha polisi) kipokelewe kama ushahidi wa upande wa utetezi.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa ombi hilo halikufuata taratibu za kisheria, kwa madai kwamba hati ya kuwasilisha haikuwasilishwa kwa mujibu wa kanuni za ushahidi.
Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali hoja hiyo baada ya majaji watatu kupitia nyaraka zote na kubaini kuwa utetezi ulitimiza masharti yote ya kisheria.
Baada ya uamuzi huo, kielelezo DE1 kilikubaliwa rasmi na Mahakama kama kielelezo cha kwanza cha upande wa utetezi ambapo mshatakiwa anajitetea mwenyewe.
Mara baada ya uamuzi huo, Lissu aliendelea kumhoji shahidi Kaaya kwa maswali ya dodoso ambapo alianza kwa kumkumbusha shahidi kuhusu maelezo aliyoyasaini polisi na kuthibitisha iwapo ni ya kwake.
Lissu: Naomba uwaeleze Waheshimiwa majaji, hayo maelezo ni yako pamoja na sahihi?
Shahidi:Nakiri haya maelezo ni yangu pamoja na sahihi.
Lissu:Unakubali yaingizwe kama kielelezo cha Mahakama?
Shahidi: Ndiyo, naomba yapokelewe kama kielelezo.
Baada ya hapo, Lissu alianza kumlinganisha shahidi huyo na ushahidi wake wa tarehe 9 Oktoba 2025 ambapo Kaaya alieleza kuwa aliajiriwa na Jeshi la Polisi mwezi Februari 2006.
Hata hivyo, katika maelezo yake ya polisi, aliandika mwaka 2005.
Lissu ambaye kitaaluma ni Mwanasheria Mbobevu aliendelea kumkaba shahidi kwa maswali kuhusu mafunzo mbalimbali ya polisi aliyodai kuyahudhuria, akitaka uthibitisho kama maelezo hayo yapo kwenye ushahidi wa maandishi.
Lissu: Uliwahi kueleza Mahakama hii kwamba ulitunukiwa cheti baada ya mafunzo ya polisi Zanzibar, kweli au si kweli?
Shahidi: Kweli.
Lissu: Je, hayo maelezo yapo kwenye ushahidi wako?
Shahidi:Hayapo.
Katika sehemu nyingine, shahidi huyo alieleza kuwa aliwahi kuhudhuria mafunzo ya “Special Sajenti” katika Chuo cha Polisi Moshi, lakini akashindwa kueleza kwa nini maelezo hayo hayakuandikwa katika taarifa zake za polisi.
-Mvutano kuhusu elimu ya Kidato cha nne ya shahidi waibuka-
Baada ya maswali ya kiutumishi, Lissu aliamua kuingia kwenye eneo la elimu ya shahidi, hatua ambayo ilizua mvutano mkali ndani ya Mahakama.
Lissu: Waeleze Waheshimiwa majaji ulisoma shule ya msingi wapi?
Shahidi:Nilisoma shule ya msingi kuanzia 1989 hadi 1995.
Lissu: Elimu ya sekondari ulianza lini?
Shahidi: Nilianza mwaka 1996 hadi 1999 katika shule ya Ryakirimu.
Kisha Lissu akauliza:
Ulipata ufaulu gani elimu ya kidato cha nne?
Swali hilo lilisababisha upande wa Jamhuri kusimama haraka kupinga, wakidai halina umuhimu kwa kesi ya uhaini na kwamba ni taarifa binafsi za mshtakiwa
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema alidai kuwa kiwango cha ufaulu wa shahidi hakina uhusiano wowote na hoja za kisheria za kesi hiyo.
Hata hivyo, Lissu alisimama na kupinga, akisema:
“Waheshimiwa majaji, kama wangetaka shahidi wao asiulizwe kuhusu elimu, basi wasingetaja historia yake ya elimu kwenye maelezo ya ushahidi. Mimi ninasaka ukweli juu ya sifa za mtu huyu ambaye amefikia ngazi ya Inspector wa Polisi.”
Baada ya mvutano wa dakika kadhaa, Mahakama ikaamua kwamba shahidi hatalazimika kujibu swali hilo.
“Mahakama inaona swali hilo halina tija katika hoja kuu ya kesi. Shahidi hatalazimika kujibu kuhusu ufaulu wake wa kidato cha nne.”-Jaji Ndunguru
Shahidi Kaaya hivyo hakujibu, na mahojiano yakaendelea.
Lissu aendeleza maswali kuhusu elimu ya juu ya shahidi ambapo aliendelea kuuliza maswali ya kielimu, akitaka kujua shahidi huyo ana sifa gani kitaaluma.
Lissu: Ulipata elimu ya kidato cha tano na sita?
Shahidi: Hapana.
Lissu:Una Advanced Diploma yoyote?”
Shahidi:Ninayo ya Refrigeration and Air Conditioning.
Lissu: Ulipata chuo gani?”
Shahidi:Interglobal College, Nairobi.
Katika hatua hiyo, shahidi alilalamika kuwa anaonewa, akidai maswali hayo yanakusudia kumdhalilisha mitandaoni, na kwenda mbali zaidi akisema wafuasi wa Chadema wamekua wakiandika kinachoendelea Mahakamani hatua kwa hatua kinyume na sheria za Mahakama wakati wa usikilizwaji wa kesi
“Maswali anayouliza mshtakiwa yana nia ya kunidhalilisha, na pia wafuasi na waandishi wa Chadema wanaweka picha zangu mitandaoni, ili nitukanwe”
Hata hivyo, Mahakama ilimkanya ikimtaka ajikite katika ushahidi wake na pia afate anachoambiwa na Mahakama
“Shahidi kuwa mtulivu. Mahakama hii ndiyo yenye mamlaka ya kulinda utu wako. Utoaji wa ushahidi si wa kumfurahisha mtu, bali kusema ukweli, jikite kwenye ushahidi wako hayo mambo ya mtandaoni achana nayo hata wakisema Mahakama si ina “Record”-amesema Jaji Ndunguru
Baada ya onyo hilo, Lissu aliendelea.
Lissu: Waeleze Waheshimiwa majaji, unafahamu chombo kinachoitwa NACTE?
Shahidi: Nafahamu.
Lissu:Chuo ulichosoma Nairobi kinatambuliwa na NACTE?
Shahidi:Kinatambulika.
Lissu:Una shahada ya chuo gani?
Shahidi:Nina Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu Huria.
Lissu:Ulisomea nini?
Shahidi: Degree ya Sheria , nilihitimu mwaka 2019.
Lissu akaendelea kuuliza iwapo shahidi huyo aliandika shahada hiyo kwenye maelezo yake polisi, naye akajibu kwamba hakuandika
Baada ya maswali kadhaa kuhusu vyuo kama Unique Academy na JR Institute of Information Technology, Lissu alimwambia shahidi:
Lissu:Nikisema wewe Inspector John Kaaya huna qualification ya kitaaluma ya chochote nitakuwa nimekosea?
Shahidi: Utakua umekosea.
Lissu kisha akamkabidhi kitabu cha Police General Orders (PGO) na kumtaka asome kipengele kinachoelezea maana ya “Professional Qualification”.
Baada ya shahidi kusoma, Lissu akasema:
Lissu: Kwa mujibu wa tafsiri hiyo, Professional Qualification ni kuwa na angalau Advanced Diploma au Shahada. Kwa hiyo kwa ushahidi wako, huna sifa hizo.
Shahidi:Sio kweli.
Katika hatua nyingine, Lissu alihamia kwenye eneo la teknolojia ya habari, akimhoji shahidi huyo kuhusu ushahidi wake uliodai kuwa video inayomuhusisha Lissu ilichapishwa kwenye Jambo TV.
Lissu: Ulisema mtu anayetumia mitandao lazima awe na jina, namba ya siri na anuani ya barua pepe?
Shahidi:Kweli.
Lissu: Na hayo maelezo yapo kwenye ushahidi wako wa maandishi?
Shahidi: Hayapo.
Lissu aliendelea kumchambua kwa undani kuhusu utaratibu wa YouTube na nani ana mamlaka ya kupakia video.
Lissu:Mtu yeyote mwenye Google Account anaweza kupakia video kwenye YouTube, siyo?
Shahidi: Kweli.
Lissu:Kwa hiyo mtu mwenye akaunti anaweza kupakia video kwenye kituo chochote kama Jambo TV?
Shahidi:Haiwezekani.
Lissu:Ni nani anayejua password ya Jambo TV?
Shahidi:Simfahamu.
Katika mazungumzo hayo, shahidi alikiri kuwa hajawahi kufanya uchunguzi maalum kubaini ni nani hasa anamiliki kituo hicho cha YouTube kilichochapisha video inayodaiwa kuwa ya Lissu.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano, Lissu alimuliza shahidi kuhusu historia yake ya kupandishwa vyeo, akitaka kuonyesha utendaji wa kawaida wa Jeshi la Polisi, ambapo kimsingi alitilia shaka juu ya hatua za upandaji wake wa vyeo
Lissu:Umesema umehudumu miaka 19 na miezi 8, umepandishwa cheo kutoka Constable hadi Inspector tu?
Shahidi:Kweli.
Lissu:Kwanini imekuchukua miaka 15 kupanda kutoka Constable hadi Inspector, wakati PGO inasema miaka 9
Shahidi:Mwajiri anajua.
Hapo Lissu akaendelea kumhoji kuhusu mfumo wa vyeo ndani ya polisi, na shahidi alikiri kuwa hajawahi kuwa Corporal wala Staff Sergeant, licha ya kuwa sasa ni Inspector.
-Kuhusu kosa la uhaini-
Lissu aliendelea kumchambua shahidi kuhusu uelewa wake wa kisheria kuhusiana na makosa yanayomhusu.
Lissu:Ulisema video hiyo ilikuwa na matamshi yenye viashiria vya jinai. Ni kosa gani hilo kwa mujibu wa sheria?
Shahidi:Sijaanisha kosa.
Lissu:Kwa kuwa unasema una shahada ya sheria, unafahamu kifungu nilichoshtakiwa nacho?
Shahidi:Nafahamu, kosa la uhaini.
Lissu: Mtu anayetangaza au kusambaza maneno ya kihaini naye ni mhalifu?
Shahidi:Inategemeana na ushahidi.
Lissu alimtaka shahidi akiri kama waandishi wa habari waliorekodi na kuchapisha video hiyo pia walitenda kosa, lakini shahidi alijibu kwa tahadhari.
Shahidi:Inategemeana na ushahidi uliopo.
Kila mara Lissu alipouliza swali lenye ukali au kuhoji utaratibu wa polisi, minong’ono ilisikika ukumbini, hasa upande wa wafuasi wa CHADEMA.
Mara kadhaa Mahakama ililazimika kutoa onyo kwa watazamaji kuacha kuingilia mwenendo wa kesi kwa kelele au tabasamu.
Hali ilikuwa ya mvutano wa kisomi huku Lissu akijaribu kutumia ujuzi wake wa sheria na uzoefu wa kisiasa, na upande wa Jamhuri ukijaribu kumkinga shahidi wao asidhoofike.
Kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu itaendelea kusikilizwa Jumatano , Oktoba 14, 2025, ambapo upande wa mshtakiwa unaojitetea mwenyewe unatarajiwa kuendelea kumuhoji shahidi wa Jamhuri maswali ya dodoso na kisha kutoa nafasi kwa upande wa Serikali kumuhoji shahidi huyo kwa kusawazisha maswali ambayo yanahitaji maelezo zaidi.
Lissu anatuhumiwa kwa kesi ya Uhaini baada ya kutoa maneno yenye viashiria vya kuhatarisha usalama wa taifa kupitia hotuba yake iliyorekodiwa Aprili 3, 2024, katika makao makuu ya CHADEMA, Mikocheni jijini Dar es Salaam, na kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo YouTube Channel ya Jambo TV.
Kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, ukikutwa na hatia hukumu yake ni kifo.