Fainali ya Ligi ya Mabingwa 2022 itachezwa jijini Paris baada ya Urusi kuvuliwa uwenyeji wa mechi hiyo kufuatia uvamizi wa taifa hilo nchini Ukraine.
Mchezo huu ulipaswa kuchezwa huko Saint Petersburg Urusi, lakini leo UEFA imesema mchezo huo umehamishwa kutokana na uvamizi wa kijeshi kati ya Urusi na Ukraiene.
Bodi inayoongoza kandanda la Ulaya baada ya kukaa kikao cha dharura imesema mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Stade de France nchini Ufaransa jijini Parisi siku ya Jumamosi, Mei 28.
Katika taarifa hiyo UEFA imetoa shukurani zake kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa msaada wake binafsi na kujitolea kuhakikisha kuwa mchezo wa soka wa klabu bingwa Ulaya uhamishwe hadi wakati wa mzozo usio na kifani utakapokwisha.
Pamoja na serikali ya Ufaransa, UEFA itaunga mkono juhudi za washikadau mbalimbali ili kuhakikisha utoaji wa uokoaji kwa wachezaji wa mpira wa miguu na familia zao nchini Ukraine ambao wanakabiliwa na mateso makubwa ya kibinadamu, uharibifu na kufukuzwa.
Hata hivyo, UEFA ilitangaza kwamba vilabu vya Urusi na Ukraine pamoja na timu ya taifa inayoshiriki katika mashindano ya kimataifa lazima zicheze mechi za nyumbani katika kumbi zisizoegemea upande wowote.
FIFA sasa inaweza kuchukua uamuzi wa kulazimisha Urusi kucheza mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Poland mnamo Machi 24 kwenye uwanja usio na upande wowote.
Spartak Moscow ndio timu pekee ya Urusi iliyosalia katika mashindano ya vilabu ya Uropa msimu huu, baada ya kufika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Europa.