Fukuto laendelea ndani ya chama cha ACT -Wazalendo

Hamad Masoud Hamad, alieykuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo

Alieykuwa  Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, Hamad Masoud Hamad, ametangaza kujiondoa katka chama hicho, licha ya kuwa bado hajakiandikia barua juu ya yeye kujiondoa.

Hamad ambaye aligombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa na kukosa nafasi hiyo, amefanya uamuzi huo akidai sababu ni chama hakina demokrasia.

Akizungumza jana na waandishi wa habari Mjini Zanzibar, kuhusu uamuzi wake, alisema  uchaguzi wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni, jijini  Dar es Salaam haukuwa huru na haki wala haukufata demokrasia kwani tayari ACT Wazalendo walishamuandaa mtu wao.

“Nilichokibaini katika uchaguzi mkuu wa uliofanyika, chama kilikuwa na mgombea wake maalum ambaye kilimuunga mkono,” alidai.

Hamadi alirudi nyuma kwa kutoa mifano wakati alipokuwa vyama vingine vya siasa na kueleza kuwa katika chaguzi zote za vyama vitatu alivyowahi kuwa mwanachama vya CCM na CUF wajumbe wote wa mkutano mkuu hawakuwa wakimpigia kampeni mgombea maalum badala yake huachiwa kupiga kura kwa mgombea wanayemtaka.

Jambo hilo limekuwa tofauti kwenye uchaguzi wa  chama cha ACT- Wazalendo, kwani Hamadi anashangazwa uchaguzi huo wajumbe walilazimishwa kumchagua Juma Duni Haji, na kwamba ni kinyume cha taratibu za uchaguzi.

Hamad licha ya kujitoa katika chama hicho lakini hajaweka msimamo wake kuhusu chama gani atakachojiunga nacho, ingawa kuna taarifa zisizothibitishwa kuwa huenda akarudi tena chama cha CUF. 

Nimeshafuatwa kujiunga na vyama zaidi ya saba, lakini bado sijaamua chama gani nitajiunga,” alisema Hamad.

Aidha alidai  kuwa awali wapenzi wengi wa Chama cha CUF waliojiunga na ACT – Wazalendo, walikuwa na imani kwamba ni chama chenye kuleta mabadiliko, lakini kumbe ni chama cha watu wachache.

Alisema hakujitoa katika chama hicho kwa sababu ya kukosa nafasi ya uenyekiti, bali ni maamuzi yake baada ya kuona chama hicho hakiendeshwi kwa ukweli na uwazi.

Aliongeza kuwa haoni sababu ya aliyekuwa makamu mwenyekiti Zanzibar Juma Duni Haji kugombea nafasi ya uenyekiti, kwa vile nafasi yake ya awali ilikuwa ikimpa nafasi ya kushiriki vikao vyote vya ndani ya chama hicho.

Wakati Hamadi akifanya maamuzi hayo wadadisi wa mambo na wanachama wengine wa vyama vya siasa, baadhi yao wanakosoa maamuzi yake, huku wakimtuhumu kuwa ni mpenda madaraka na si mpenda haki, na hii ni baada ya kukosa cheo.

Wengine wanasema huenda akafilisika kisiasa, kwani pamoja na kuwa ni haki ya kila mtu kuchagua chama anachokitka lakini kwa ndugu Hamadi ni kama amejiweka katika makaa ya moto.

Hamadi Masoud Hamad amesisitiza kuwa suala la yeye kujiondoa kwa kutamka ndio msimamo wake na hiyo haitabadilisha mawazo yake kwani ataandika barua rasmi ya kujiondoa.

“Japo sijaandika barua rasmi ya kujiengua katika chama, lakini ibaki kuwa kauli yangu hii inatosha kukihama chama hicho,” alisema.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu ACT-Wazalendo Zanzibar, Salum Bimani, alisema uchaguzi uliofanyika ndani ya chama mwezi uliopita wa kumpata Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ulifanyika kwa huru na haki na kabla ya uchaguzi huo kufanyika ulitoa fursa kwa kila mwanachama kuchukua fomu na kila mgombea kunadi sera zake mbele ya vyombo vya habari.

Wakati Bimani akisema hayo hivi Februali Mosi 2022, Mwenyekiti Taifa wa chama cha ACT -Wazalendo, ndugu Juma Duni Haji aliwaambia wanahabari kuwa hana ugomvi na Hamad kuhusu yeye kushinda nafasi hiyo, kwani hata aliposhinda Hamadi alimpongeza kwa ushindi huo.

Babu Duni pia liongeza na kusema kuhusu suala la demokrasia ndani ya chama hicho ni suala ambalo linazingatiwa huku akitolea mfano namna ambavyo walifanya mkutano mkuu wa chama hicho uliowekwa wazi bila kificho kwa kushirikisha watu wa makundi mbalimbali, huku wafadhili wa mkutano huo kwa kiasi kikubwa wakiwa ni wanachama wenyewe ambao walichangia pesa kufanikisha shughuli hiyo.

Salum Bimani ameongeza kuwa ni vyema Hamad akukubali kwamba kura hazikutosha kupata nafasi hiyo dhidi ya mgombea mwenzake Juma Duni Haji na chama kilitoa nafasi kwa mtu kufuata taratibu za kukata rufani kama hakuridhika na matokeo.

Alimpongeza mwanachama huyo kwa kutumia demokrasia yake ya kutoka ndani ya chama na kumtakia safari njema huko aendako.

Si Hamad pekee ndiye aliyoondoka ACT Wazalendo wapo wanachama kadhaa ambao hivi karibuni wametangaza kujiondoa ndani ya chama hicho ambapo hadi sasa hawajaweka wazi wanakwenda chama gani.

Hamadi Masoud Hamadi, aliyezaliwa mwaka 1957, alijiunga na ACT- Wazalendo mwaka 2019 akitokea Chama cha Wananchi CUF, wakati ambapo marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alipotangaza kuachana na CUF na kisha kuingia ACT-Wazalendo.

https://youtu.be/kHz9p1d82DI
Sikiliza alichokisema Hamad Masoud