Fukuto ndani ya TLS lazidi kuongezeka, Mawakili waamua kuishtaki

Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Kanda ya Ziwa, Steven Kitale amefungua shauri la mapitio ya kimahakama dhidi ya TLS.

 

Shauri hilo namba 16018/2024, lililofunguliwa katika  Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza mnamo tarehe 3 July 2024, mbele ya Jaji Athuman Matuma limewashtaki Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), mkurugenzi mtendaji wa TLS, kamati ya uongozi wa chama hicho pamoja na Mwanasheria Mkuu.

 

Wakili Kitale ameiomba Mahakama impe ruhusa kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama pamoja na amri ya muda ili kuzuia mkutano mkuu wa mwaka (AGM) 2024 ambao unatarajiwa kufanyika mwezi ujao.

 

Katika maombi yake ameweka zuio la mchakato wa uchaguzi, kupinga uteuzi na uwepo wa baadhi ya wajumbe katika Kamati ya Uchaguzi ambayo ilipitisha majina ya wagombea.

 

Imeelezwa kuwa baadhi ya wajumbe hawakukidhi viwango vya kuteuliwa na uteuzi umefanywa bila ya kushirikisha wajumbe wote wa Kamati ya Uongozi.

 

Wajumbe wanaodaiwa kwa mujibu wa mashtaka kutohusiha leseni zao ni pamoja na Mheshimiwa Robert Vincent Makaramba, ambaye amedai leseni yake ya uwakili haijahuishwa tangu tarehe 1 Aprili 2021 na Wakili Sakina Hussein Sinda, ambaye hajahuisha leseni yake ya uwakili tangu tarehe 31 December 2018.

 

Vilevile mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi Jaji Mstaafu Joaquine Antonette De-Mello inadaiwa kuwa hafanyi kazi za uwakili kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizopo.

 

Hivyo kutokana na hali hii, Wakili Kitale amedai kuwa imeibua maswali makubwa kuhusu uhalali wa uteuzi wa Kamati hii ya Uchaguzi na mchakato mzima wa Uchaguzi.

 

Katika ombi lake Kitale amebainisha kuwa mbali na hilo la baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi kukosa sifa, hoja nyingine itakayojadiliwa katika shauri hilo ni pamoja na kupandishwa kwa ada ya usajili wa washiriki wa mkutano mkuu wa TLS kutoka shilingi 118,767 na shilingi 100,000 kwa washiriki wa mtandaoni hadi shilingi 200,000, uamuzi ambao amedai haukupitishwa na baraza la uongozi la chama hicho na kufanywa nje ya utaratibu.

 

Ikumbukwe kuwa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kwa sasa imegubikwa na mgogoro mwingine baada ya mgombea Boniface Mwabukusi kuondolewa katika orodha ya wagombea wa urais na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa chama hicho. Mwabukusi ameshapeleka shauri mahakamani kupinga maamuzi haya.