Gambia imeripoti mlipuko wa ugonjwa wa mpox siku ya Jumanne baada ya kugunduliwa kwa kisa kimoja kupitia mfumo wa kawaida wa ufuatiliaji wa magonjwa, huku nchi kadhaa jirani zikiripoti ongezeko la maambukizi hivi karibuni.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesisitiza mwezi uliopita kuwa mpox bado ni dharura ya kiafya ya kimataifa, kutokana na kuongezeka kwa visa katika ukanda wa Afrika Magharibi.
“Visa vya mpox vimegunduliwa nchini kupitia mfumo wa kawaida wa ufuatiliaji,” lilisema tamko kutoka Wizara ya Afya ya Gambia, na kuongeza kuwa kisa hicho kiligunduliwa siku ya Ijumaa.
“Tukio la kugundua kisa kimoja katika nchi ambako ugonjwa huo haukuwa unaripotiwa kwa sasa linachukuliwa kama mlipuko, unaohitaji hatua za haraka,” iliongeza wizara hiyo.
Wizara imesema inatekeleza juhudi za kutafuta visa zaidi, kufuatilia watu waliokaribiana na mgonjwa, pamoja na kuelimisha jamii ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Mpox unasababishwa na virusi vinavyotokana na familia moja na ile ya ndui. Unaweza kuambukizwa kwa binadamu kupitia wanyama walioambukizwa, lakini pia huweza kuenea kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia mgusano wa karibu wa kimwili.
Ugonjwa huu, ambao ulionekana kwa mara ya kwanza kwa binadamu mwaka 1970 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, husababisha homa, maumivu ya misuli na upele mkubwa unaofanana na majipu, na unaweza kuwa hatari kwa maisha.
Mpox una makundi mawili ya virusi: clade 1 na clade 2. Wizara imesema inaendelea na uchunguzi wa kijenetiki (sequencing) ili kubaini aina ya virusi vilivyogunduliwa nchini Gambia.
Kuanzia Januari hadi mwishoni mwa Mei mwaka huu, nchi jirani ya Sierra Leone iliripoti jumla ya visa 3,350 vya mpox, vikiwemo vifo 16. Nchini Liberia, visa 71 vilikuwa vimeripotiwa kuwa bado hai kufikia mapema Juni, kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Umma ya nchi hiyo.
Guinea, kwa upande wake, ilitangaza wiki iliyopita kuwa idadi ya visa vya mpox ndani ya mipaka yake tangu ugonjwa huo ulipogunduliwa Septemba mwaka jana imezidi 200.
Maelfu ya visa vimeripotiwa pia mwaka huu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Burundi, kwa mujibu wa taarifa za WHO.