Jeshi la polisi nchini Kenya limetumia mabomu ya machozi leo Alhamisi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakilaani mauaji ya mwalimu mmoja aliyefariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi, hali iliyotishia kufunika juhudi za serikali kuwasilisha bajeti mpya bila kuchochea ghasia kama za mwaka uliopita.
Serikali ya Kenya imeandaa kwa umakini mkubwa muswada wake mpya wa bajeti kwa lengo la kuepuka maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa mwaka 2024, ambapo kupandishwa kwa kodi kulisababisha hasira ya wananchi na vurugu kubwa.
Hata hivyo, kuuawa kwa Albert Ojwang, mwalimu mwenye umri wa miaka 31, akiwa korokoroni baada ya kukamatwa kwa kuchapisha ujumbe wa kumkosoa afisa mwandamizi wa polisi mtandaoni, kumechochea upya hasira kuhusu ukatili wa polisi nchini humo.
“Huwezi kumuua mmoja wetu akiwa gerezani kisha mtarajie tuwe kimya,” alisema Tiffany, mwanaharakati mwenye umri wa miaka 22 aliyekuwa akishiriki maandamano katika eneo la biashara la Nairobi.
Mamia ya waandamanaji walikuwa wamegawanyika katika makundi madogo katikati ya jiji la Nairobi, wengine wakirusha mawe kwa polisi ambao walijibu kwa mabomu ya machozi.
Takriban magari mawili yalichomwa moto, huku watu watatu wakijeruhiwa kwa risasi za mpira, mmoja wao alipelekwa hospitalini.
Ingawa ghasia hizo hazikufikia kiwango cha mwaka jana, ambapo maelfu walivamia bunge tarehe 25 Juni na kumlazimu Rais William Ruto kufuta muswada wa kodi hali bado ilikuwa tete.
Katika maandamano hayo ya 2024, watu wasiopungua 60 walipoteza maisha, huku makundi ya kutetea haki yakiripoti kuwa makumi ya wengine walikamatwa kiholela na vyombo vya usalama.
Kenya, ambayo ni mojawapo ya sehemu ya kitovu cha uchumi kwa Afrika Mashariki, imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiuchumi zikiwemo gharama kubwa ya maisha, ukosefu wa ajira na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Katika bajeti mpya, serikali imejikita zaidi katika kuongeza mapato kwa kulenga kodi kwa makampuni badala ya walaji wa kawaida.
Waziri wa Fedha John Mbadi alikiri kuwa maandamano ya mwaka jana yalionyesha umuhimu wa utawala bora na ushirikishwaji wa wananchi.
“Ili kupata imani ya wananchi, tumeimarisha ushiriki wa umma katika utungaji wa sera zote, ikiwemo mchakato wa maandalizi ya bajeti,” alisema Bwana Mbadi, akitaja jukwaa jipya la mtandaoni linalowezesha wananchi kutoa maoni yao.
Hata hivyo, mwezi uliopita, kukamatwa kwa mbunifu wa programu aliyesanifu tovuti iliyokosoa bajeti na kuruhusu wananchi kuwasilisha malalamiko yao moja kwa moja kwa serikali, kulitibua zaidi hali ya mambo.
Gharama na Changamoto za Kiuchumi

Kenya inakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni, ambapo malipo ya riba pekee yanazidi bajeti za afya na elimu kwa pamoja. Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema bajeti ya mwaka huu huenda isisababishe hasira kama mwaka jana, lakini bado ina changamoto zake.
Bajeti hiyo inalenga kuongeza mapato kwa kupunguza matumizi ya serikali na kuziba mianya ya upotevu wa kodi, ingawa wakosoaji wanasema ina ongezeko la gharama zisizo za moja kwa moja ambalo linaweza kudhuru biashara ndogo.
“Muswada wa mwaka huu wa fedha, ukilinganishwa na wa mwaka jana, umeepuka makali ya mgogoro,” alisema Patricia Rodrigues, mchambuzi wa taasisi ya kimataifa ya Control Risks.
“Lakini bado unahusisha ongezeko la kodi kwenye mapato na michango ya kijamii, na kuondoa misamaha ya kodi kwa biashara ndogo na za kati,” aliongeza.
Katika mazingira magumu ya kiuchumi duniani, Benki ya Dunia imeshusha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Kenya kutoka asilimia 5.0 hadi 4.5 kwa mwaka 2025.
Hali ya haki za binadamu nayo imezidi kuwa chanzo cha sintofahamu. Ojwang, aliyekamatwa kwa kumkosoa Naibu Mkuu wa Polisi Eliud Kipkoech Lagat, ni mfano mpya wa madai ya ukiukaji wa uhuru wa kujieleza.
“Tunataka Naibu Mkuu wa Polisi ajiuzulu na kisha akamatwe,” alisema Anami Daudi Toure, mwanaharakati mwenye umri wa miaka 27 aliyeshiriki maandamano hayo.