Shahidi wa tatu wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Amani Golugwa, amemaliza kutoa ushahidi wake baada ya kuhojiwa kwa maswali ya dodoso na mawakili wa Serikali.

Katika mahojiano hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nasoro Katuga, alimuuliza shahidi kuhusu kauli mbalimbali zinazodaiwa kutolewa na Lissu katika mkutano wa Aprili 3, 2025, ikiwemo kauli ya “tunaenda kuzuia uchaguzi” na kama kauli hiyo inaweza kutafsiriwa kama sentensi kamili yenye maana.
Golugwa ambaye ametumia siku nne tangu aanze kutoa ushahidi wake mahakamani, alikubaliana na Katuga kwamba kauli hiyo ni sentensi kamili, lakini katika maswali mengine alijibu kuwa hakumbuki baadhi ya kauli zinazodaiwa kutolewa na Lissu, ikiwemo kuhusu majaji kuwa “MaCCM”, “mahakamani hakuendeki” na polisi kuingiza kura feki na vibegi mgongoni.
Shahidi huyo pia alipinga hoja kwamba vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 zilisababishwa na kauli za Lissu. Alisema si kweli, akieleza kuwa chama kilizuiwa kufanya shughuli zake za kisiasa na kwamba hotuba ya Lissu ilitolewa kabla ya uchaguzi.
Katika hatua nyingine, Golugwa alisema alisikia taarifa kuhusu vurugu siku ya uchaguzi, lakini hakukubaliana na hoja kwamba vurugu hizo zilisababishwa na kauli za Mwenyekiti wa Chadema.
Akijibu maswali ya Wakili wa Serikali, Ajuaye Nzegeli, Golugwa alikubaliana kwamba Rais na wabunge hupatikana kupitia uchaguzi na kwamba uchaguzi unapovurugika viongozi hao hawawezi kupatikana. Pia alikiri kufahamu maana ya neno “mubashara”, akisema linamaanisha kurusha tukio moja kwa moja.
Baada ya kumaliza kuhojiwa na upande wa Jamhuri, Golugwa aliulizwa maswali ya ufafanuzi na Lissu kuhusu baadhi ya majibu aliyoyatoa wakati wa dodoso.
Katika ufafanuzi huo, Golugwa alisisitiza msimamo wake kuhusu kauli ya Chadema ya “No Reform, No Election”, akisema haikuwa na maana ya kuzuia watu kwenda kupiga kura, bali kuwaelewesha wananchi kwamba uchaguzi usio wa haki si uchaguzi na kuwaacha wafanye maamuzi baada ya kuelewa hali hiyo.
Golugwa pia alifafanua kauli yake ya awali kwamba kesi inayomkabili Lissu ni ya uongo. Alisema alimaanisha kuwa katika kesi hiyo Lissu ndiye mshtakiwa pekee na kwamba hakukuwa na mtu mwingine aliyechochewa, ndiyo maana aliona kesi hiyo ni ya uongo.
Kuhusu ripoti ya Tume ya Uchunguzi kuhusu matukio ya baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, Golugwa alisema hakubaliani na ripoti hiyo kwa ujumla wake, licha ya kukiri kwamba baadhi ya sababu zilizotajwa kuhusiana na machafuko ni za kweli.
Alisema kutokubaliana kwake kulitokana na baadhi ya mambo aliyoyaona hayakuakisi uhalisia, ikiwemo taarifa kuhusu watu kutekwa, kupotea na baadhi ya watu kuuawa.
Golugwa pia alieleza namna alivyopatikana kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, akisema Mwenyekiti ndiye anayependekeza jina ambalo baadaye hupelekwa Baraza Kuu kwa ajili ya kuthibitishwa.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi, shahidi huyo alisisitiza kuwa uteuzi wa wajumbe wa Tume hauko huru kwa sababu unafanywa na mtu mmoja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hali aliyosema inafanya wajumbe hao kuwa chini yake kwa kuzingatia muundo wa uteuzi huo.
Aidha, Golugwa alisema hakusikia baadhi ya kauli zilizodaiwa kutolewa na Lissu katika hotuba ya Aprili 3, 2025, na kwamba ushahidi alioutoa ulitokana na mambo ambayo yeye mwenyewe aliweza kuyasikia.
Hapa chini ni sehemu ya maswali na majibu yaliyojiri mahakamani:
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama sentensi “tunaenda kuzuia uchaguzi” je, ni sentensi kamilifu yenye kuleta maana au si kamilifu?
Golugwa: Ni sentensi kamilifu.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kwenye hotuba, je, ulimsikia Mwenyekiti akisema Majaji ni MaCCM?
Golugwa: Hilo sikumbuki, pengine aulizwe yeye mwenyewe.
Katuga: Ulimsikia akisema mahakamani hakuendeki?
Golugwa: Sikumbuki.
Katuga: Je, ulimsikia akisema kwamba polisi wanaingiza kura feki na vibegi mgongoni?
Golugwa: Sikumbuki.
Katuga: Sasa wewe uliyoyasema kuhusiana na hotuba ya Mwenyekiti kwenye mkutano wa tarehe 3 Aprili ni maneno yote au ni kati ya yale aliyozungumza?
Golugwa: Nimeyasema yale ambayo mimi nimeweza kuyasema.
Katuga: Hujui au unajua kama kuna mengine aliyozungumza?
Golugwa: Sifahamu.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama vikao vyenu vinakuwa na maazimio.
Golugwa: Waheshimiwa Majaji, kwa kawaida huwa na maazimio.
Katuga: Kama nilikusikia neno “kukinukisha”, ulilisikia?
Golugwa: Ndiyo.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kwamba neno “kukinukisha” ni kitendo.
Golugwa: Inategemeana na matumizi ya hilo neno.
Katuga: Ni ushahidi wako kwamba Jumuiya ya Ulaya walisikitishwa na vurugu za siku ya uchaguzi?
Golugwa: Ni kweli nilisema.
Katuga: Unakumbuka kwamba Mwenyekiti alisema wataenda kuuvuruga uchaguzi?
Golugwa: Ninakumbuka.
Katuga: Sasa waambie Waheshimiwa Majaji kwamba siku hiyo ya uchaguzi vurugu zilitokea.
Golugwa: Niliskia kulikuwa na vurugu.
Katuga: Ni kweli kwamba zile vurugu zilitokana na kauli za Mwenyekiti?
Golugwa: Si kweli.
Katuga: Unafahamu au hufahamu kwamba mshtakiwa anashtakiwa kwa kutoa na kuchapisha maneno hayo ya “tunaenda kuvuruga uchaguzi” na mengineyo?
Golugwa: Ninafahamu.
Katuga: Katika mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025, baada ya malalamiko mengi, mshtakiwa alikuja au alitangaza maazimio kwamba “tunaenda kuzuia uchaguzi”?
Golugwa: Mheshimiwa, hakukuwa na kikao cha maazimio, kwa hiyo hakukuwa na maazimio yoyote.
Katuga: Unajua ama hujui kwamba kwa sheria zetu za uchaguzi mshindi anapatikana kwa kura nyingi?
Golugwa: Kama uchaguzi unakuwa wa haki na huru ni sawa.
Katuga: Ni kweli ama si kweli kwamba Mwenyekiti alipokamatwa, Makamu Mwenyekiti aliendeleza hiyo nia ya kuzuia uchaguzi?
Golugwa: Makamu Mwenyekiti aliendeleza maazimio ya chama.
Katuga: Sasa waambie Waheshimiwa Majaji kwamba Bwana Heche aliwahi kufanya interview na East Africa Radio.
Golugwa: Sifahamu.
Katuga: Ulisikiliza hotuba yote ya Jaji Chande kuhusiana na ya Oktoba 29?
Golugwa: Nilisikia vipande vipande.
Katuga: Ulimsikia akisema kwamba zile vurugu zilitokana na kauli za wanasiasa?
Golugwa: Sikuskia.
Nzegeli: Ni kweli kwamba viongozi kama Rais na wabunge wanapatikana kwa kuteuliwa?
Golugwa: Ni kweli.
Nzegeli: Ni kweli kabisa uchaguzi ukivurugika viongozi hawa hawapatikani?
Golugwa: Ni kweli.
Nzegeli: Nitakuwa sahihi nikisema waandishi wa habari wakirusha mubashara wanakuwa hawana nafasi ya kuchuja wala kupunguza?
Golugwa: Hilo Waheshimiwa Majaji, waandishi wanaweza kuwa na majibu mazuri.
Nzegeli: Unajua neno mubashara lina maana gani?
Golugwa: Nalijua, lina maana ya kurusha moja kwa moja.
Maswali ya ufafanuzi
Lissu: Shahidi uliulizwa mahakamani kuhusiana na uchaguzi wa udiwani, kilichotokea kwenye uchaguzi, na ukaulizwa kwamba kama mlikwenda mahakamani, ukasema hamkuona haja ya kwenda mahakamani. Nahitaji ufafanuzi hapo.
Golugwa: Kweli kulikuwa na malalamiko yaliyotokana na matatizo ya uchaguzi huo wa madiwani, lakini tuliona matatizo haya yanahitaji kushughulikiwa kisiasa na si mahakamani.
Lissu: Uliulizwa vilevile uchaguzi wa 2024 wa mitaa, vitongoji na vijiji na ukaulizwa kuhusiana na utaratibu wa kupeleka malalamiko kwenye kamati za rufaa, ukajibu kwamba rufaa zote zilikataliwa kutokana na uhuni na ushenzi uliofanywa na ndiyo maana hatukwenda mahakamani.
Golugwa: Kwa idadi ya wagombea walioenguliwa kwa kiwango chao na kama kesi zilikuwa nyingi sana, ndiyo maana tuliona kwamba matatizo hayo yanahitaji kumalizwa kisiasa na si mahakamani.
Lissu: Uliulizwa kuhusiana na hotuba ya Jaji Chande na ukaulizwa kama unaamini, ukasema hukubaliani nayo yote. Naomba fafanua.
Golugwa: Niliposema siiamini hotuba ya Jaji Chande ni kutokana na baadhi ya mambo niliyoyasikia niliona hayakisi uhalisia, ikiwemo taarifa ya watu kutekwa na kupotea.
Lissu: Ukaulizwa pia kwa hiyo hata sababu za machafuko huziamini, ukasema sababu za machafuko ni za kweli lakini sikubaliani na hotuba kwa ujumla wake. Kwa nini unasema sababu za machafuko ni za kweli lakini ripoti haukubaliani nayo kwa ujumla wake?
Golugwa: Sikubaliani na hotuba kwa ujumla kutokana na sehemu ya ripoti ile kutokuwa na ukweli, ikiwemo baadhi ya watu waliouawa.
Lissu: Uliulizwa juu ya nafasi yako ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama, kilichotokea mpaka ukawa Naibu Katibu Mkuu. Majibu yako ulisema Naibu Katibu Mkuu anapendekezwa na Mwenyekiti na anateuliwa na Baraza Kuu. Akaendelea kukuuliza kwamba si ulichaguliwa na Mwenyekiti, ukasema anachaguliwa na Mwenyekiti lakini anathibitishwa Baraza Kuu. Fafanua hapo.
Golugwa: Ili uweze kuwa Naibu Katibu Mkuu inatakiwa Mwenyekiti ateue jina na kisha linapelekwa Baraza Kuu ambalo lenyewe linathibitisha.
Lissu: Uliulizwa kama kwa msimamo huo wa No Reform No Election ulilenga kuzuia mtu yeyote kwenda kuzuia uchaguzi, ukajibu kwamba sisi hatukuzuia mtu yeyote kwenda kuzuia uchaguzi.
Golugwa: Nilikuwa na maana kwamba tuwaeleze watu waelewe kwamba uchaguzi usio wa haki si uchaguzi. Watu wakishaelewa wafanye maamuzi.
Lissu: Shahidi, unakumbuka ulitoa ushahidi kuhusiana na kuenguliwa kwa wagombea wa Chadema na ukasema hujawahi kuona mgombea wa CCM akienguliwa na Tume ya Uchaguzi, halafu ukaambiwa kwamba useme kama ulipokea taarifa ya Tume kwamba wagombea walioenguliwa CCM walienguliwa?
Golugwa: Taarifa za kuenguliwa wagombea zinakuwepo kwenye ofisi ya Tume.
Lissu: Uliulizwa sana kuhusiana na maandamano, ukaulizwa maandamano si lazima yalete bughudha kwa watu, ukasema ni kweli lazima yalete bughudha kwa watu fulani.
Golugwa: Ni kweli yanaleta bughudha kwa wanaochukia kusikia ujumbe, yanaleta bughudha kwa wanaokaa barabarani.
Lissu: Unakumbuka ulisema kwamba hii kesi ni ya uongo kwamba mtu mmoja hawezi kufanya uhaini? Waeleze Waheshimiwa Majaji kwamba ulikuwa na maana gani.
Golugwa: Nilikuwa namaanisha kwamba kwenye kesi hii mshtakiwa yupo peke yake, hakuna aliyechocheka, kwa hiyo ndiyo maana niliona kesi hii ni ya uongo.
Lissu: Shahidi uliulizwa juu ya Tume ya Uchaguzi, ukaonyeshwa Ibara ya 74 ya Katiba na Ibara ya 74(1) kuhusiana na uteuzi wa wajumbe wa Tume. Kwenye majibu yako ukasema huo uteuzi huru wa Tume haupo kwa sababu huo mfumo umeegemea upande mmoja.
Golugwa: Uteuzi huo wote unafanywa na mtu mmoja ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano na hivyo wale watu wanakuwa chini yake kwa maana ya muundo jinsi ulivyo.
Lissu: Uliulizwa kuhusiana na mkutano wa tarehe 3 Aprili, kuhusiana na mimi. Ulisema kwamba ulinikaribisha kwenye mkutano lakini hukuniandikia hotuba. Ulipoulizwa ulijua mambo yaliyokuwa kichwani mwake ukasema ndiyo. Ulikuwa na maana gani?
Golugwa: Sekretarieti iliandaa mkutano wa watia nia waje kuelimishwa kuhusu msimamo wa No Reform No Election na nilichojua alikuwa anakuja kuzungumzia kuhusu huo msimamo.
Lissu: Uliulizwa kwamba nikisema “Majaji ni MaCCM” na nikisema kwamba “mahakamani hakuendeki” na nikisema kwamba “mapolisi wanabeba vibegi vya kura”, ukaulizwa kwamba wewe umesikia yale uliyotaka kusikia?
Golugwa: Ni kwamba kile nilichokisema kinatokana na kile ambacho nimesikia.
Lissu: Umeulizwa juu ya vurugu za uchaguzi mkuu wa 2025, ukasema kwamba ni kweli kulikuwa na vurugu. Ukaulizwa kwamba Lissu alisema anakwenda kuvuruga uchaguzi. Sasa si kweli kwamba Lissu ndiye sababu? Ukasema si kweli kwa sababu chama kilizuiwa.
Golugwa: Nilisema hivyo kwa sababu chama kilizuiwa kufanya shughuli zake za kisiasa na hotuba ya Lissu ilitolewa kabla ya uchaguzi.