Tetemeko la ardhi limesababisha taharuki katika maeneo ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida kwenye mpaka kati ya Singida na Dodoma yakiwa na ukubwa wa 4.3 na 4.9 katika kipimo cha richer.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Mjiolojia Mwandamizi kutoka Taasisi ya Jiolojia na na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Gabriel Mbogoni alisema kuwa Februari 16, mwaka huu saa 12.13 jioni tetemeko lenye ukubwa wa Richert 4.9 lilitokea katika eneo la Makuru, Tarehe 17 Februari, saa 1:45 asubuhi tetemeko lenye ukubwa wa richer 4.3 lilitokea eneo la Makuru na Feburari 17, mwaka huu tetemeko lenye ukubwa wa richer 4.9 lilitokea katika eneo la Zuboro.
Alisema kuwa matukio hayo yalisikika katika maeneo ya mkoa wa Dodoma na Singida, hata hivyo pamoja na matetemeko hayo kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani, GST haijapata taarifa zozote za kutokea kwa madhara kutokana na matetemeko hayo.
Alisema kuwa Mikoa ya Dodoma na Singida imepitiwa na ukanda wa bonde la ufa Afrika Mashariki mkondo wa mashariki.
“Mikoa mingine katika mkondo wa Mashariki ni Manyara, Arusha, Mara, Iringa na Njombe ambapo mkondo wa magharibi una mikoa ya Kagera, Kigoma,Katavi, Rukwa Songwe, Mbeya na Ruvuma, maeneo ya ukanda wa bonde la Ufa kwa kawaida ni maeneo tete ya mabadiliko ya kijiolojia ambayo hukumbwa na matetemeko ya ardhi na milipuko ya volcano, “ alisema
Alisema kuwa matetemeko ya ardhi hutokana na nguvu za asili ambazo husababisha mgandamizo katika matabaka ya miamba.
.“Mpaka hivi sasa haijagunduliwa teknolojia ya kuweza kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi, hivyo GST inatoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari muda wote kama ambavyo imekuwa ikishauriwa ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na majanga ya asili ya jiolojia ikiwemo matetemeko ya ardhi, mojawapo ni hatua ya tahadhari dhidi ya tetemeko la ardhi.”
Alisema tahadhari hizo ni pamoja na kujenga nyumba imara kwa kuzingaria viwango halisi vya ujenzi, kupata ushauri wa kiutaalam wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa kulingana na jiolojia ya eneo husika, kuepuka ujenzi katika miinuko yenye kuambatana na mawe, miamba na mipasuko ya miamba.
“Wakati wa tukio kama uko nje ya jengo unashauriwa kubaki nje, simama mahali pa wazi mbali na majengo marefu, miti mirefu, nguzo na nyaya za umeme na ujikinge kichwani kadri inavyowezekana.”
Álisema kuwa endapo tetemeko linatokea ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa kubaki ndani na ukae sehemu salama kama vile chini ya uvungu wa meza imara, kitanda ama simama kwenye makutano ya kuta mbali na madirisha, makabati ya vitabu, vyombo au samani ili kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo.