Jeshi la Polisi limepanga kuandaa hafla maalum kwa ajili kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro baada ya kustaafu utumishi wa Jeshi hilo.
Taarifa iliyotolewa leo Mei 9, 2023 na msemaji wa jeshi hilo, David Misime imeeleza kuwa sherehe za kumuaga Siro zitafanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA) kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam Mei 10, 2023 kuanzia saa 1 asubuhi.
Taarifa hiyo imeeleza kutakuwa na gwaride maalum la kumuaga ikiwa ni utaratibu wa Jeshi la Polisi kuwaaga kwa gwaride maalum viongozi wa Polisi waliofikia cheo cha Kamishna wa Polisi na Inspekta Jenerali wa Polisi
IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro amelitumika Jeshi la Polisi kwa miaka 30 tangu Februari 19, 1993 alipojiunga rasmi hadi kustaafu mwezi Machi 2023 na ni Mkuu wa Jeshi la Polisi wa 10 kuliongoza jeshi hilo tangu uhuru na ameliongoza kuanzia tarehe Mei 28, 2017 hadi Julai 20, 2022.