Mawakili wa upande wa utetezi kesi namba mbili ya mwaka 2022, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuwa hali ya Sabaya ni mbaya baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kichwa Julai 27 mwaka huu.
Sabaya na wenzake wanne wanakabiliwa na mashtaka saba likiwamo la uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya ofisi wakati akiwa Mkuu wa wilaya hiyo.
Juni Mosi mwaka huu, Sabaya na wenzake wanne walipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashtaka yanayowakabili mbele ya hakimu mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey.
Hata hivyo Sabaya ambaye ni mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo alifikishwa mahakamani hapo leo kichwa chake kikiwa kimeviringishwa bandeji huku mkononi akiwa na kifaa cha kuchomekea dripu.
Awali wakili wa Sabaya, Fridolin Bwemelo aliieleza mahakama hiyo kuwa Sabaya amefanyiwa upasuaji mkubwa wa kichwa kutokana na uvimbe aliokuwa nao na kwamba anahitaji kupata uangalizi wa karibu.
“Sabaya amefanyiwa upasuaji mkubwa wa kichwa na sio upasuaji mdogo hivyo anahitaji apate huduma muhimu na uangalizi wa karibu,”
Wakamtaka mwendesha mashtaka wa kesi hiyo kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo kwa kuwa walishaieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi umekamilika.
Wakili upande wa mashtaka Sabitina Mcharo aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba wanasubiri kibali kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali cha kuipa uwezo mahakama hiyo kuendelea kuisikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo Hakimu mkazi wa mahakama hiyo aliyekuwepo, Elibariki Philly aliahirisha kesi hiyo mpaka Agosti 12 mwaka huu.