Search
Close this search box.
Africa

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha leo inatarajia kutoa uamuzi katika kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabya na wenzake sita iwapo wana kesi ya kujibu au la.

Mnamo Januari 10, Hakimu Mkazi Patricia Kisinda ambaye anasikiliza kesi hiyo alisema leo Januari 14 Mahakama hiyo itatoa uamuzi huo baada ya upande wa Jamhuri kufunga kesi kwa upande wao

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule aliieleza kuwa shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa ila upande wa Jamhuri wanaomba kufunga kesi dhidi ya washtakiwa hao.

Wakili wa utetezi, Mosses Mahuna alieleza kuwa hawana pingamizi na ombi lililowasilishwa  licha ya wao kuwa na fursa ya kufanya mawasilisho kushawishi mahakama endapo watuhumiwa wana kesi ya kujibu au la, hawatatumia fursa hiyo.

“Kiutaratibu mahakama inapaswa ku determine watuhumiwa kama wana kesi ya kujibu au la, na kwa upande wetu tuna haki ya kuleta submissions ili kuieleza na kushawishi mahakama endapo wana kesi ya kujibu au la” alisema Wakili Mahuna na kuongeza kuwa 

“Upande wetu hatutatumia hali hiyo, tunaomba kuiachia mahakama ili yenyewe ipitie vielelezo na mwenendo na kusema kama wana kesi ya kujibu au la,” alisema. Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 13 na vielelezo 12.

Mbali na Sabaya, washtakiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya ambao wanakabiliwa na makosa matano.

Shtaka la kwanza wanadaiwa mnamo Januari 22, 2021, waliongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linalowakabili washtakiwa wote saba kwamba walipokea shilingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso, huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Kosa la pili, tatu na nne Sabaya pekee anadaiwa kujihusisha na rushwa na kwamba alichukua shilingi milioni 90, matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Ikumbukwe kuwa wakati uamuzi huu ukisubiriwa hii leo, tayari Sabaya alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, hukumu ambayo ilitolewa Oktoba 15, 2021

Sabaya na wenzake kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Juni 4, 2021 baada ya kukamatwa Mei 27 wilayani Kinondoni jijini Dar es salaam, na kesi hiyo ikaanza kusikilizwa Septemba 23, 2021.

Comments are closed